NAIBU WAZIRI AUAWA LIBYA

Naibu Waziri wa viwanda nchini Libya ameuawa kwa kupigwa risasi wakati alipokuwa ziarani mjini Sirte Mashariki mwa Tripoli ambako alizaliwa.

Vyombo vya habari nchini humo vinasema kuwa watu wasiojulikana walimfyatulia risasi kadhaa Hassan al-Droui karibu nasoko rasmi mjini humo.

Ni mauaji ya kwanza ya afisaa wa serikali ya mpito ya Libya.

Libya imekuwa ikikumbwa na vurugu tangu kuondolewa mamlakani kwa hayati Muammar Gaddafi mwezi Oktoba mwaka 2011.

Sirte ilikuwa ngome ya mwisho ambako mapigano yalitokea wakati wa harakati za mapinduzi ya Muamar Gaddafi ambaye alikamatwa na kupigwa risasi akijaribu kujificha kutoka kwa waasi.

Bwana al-Droui alikuwa mwanachama wa zamani wa baraza la mpito lililosimamia kipindi cha mpito baada ya Gadaffi kuuawa.

Aliteuliwa kama naibu waziri na waziri mkuu wa kwanza wa mpitona kuendelea kushikilia wadhifa huo hata baada ya Ali Zeidan kuchukua mamlaka.