MJI WA BOR WAKOMBOLEWA TENA

Jeshi la Sudan Kusini linasema limeukomboa mji wa Bor kutoka kwa waasi.

Msemaji wa jeshi, Philip Aguer, alieleza kuwa wanajeshi wa serikali wamewashinda waasi kama 15,000 watiifu kwa makamo wa rais wa zamani, Riek Machar.

Bor, mji mkuu wa jimbo la Jonglei, umekombolewa na kurejea mikononi mwa waasi mara kadha katika vita vya mwezimmoja.

Maelfu ya watu wako mbioni wanajiepusha na mapigano.

Mwandishi wa BBC mjini Juba anasema jeshi sasa linaweza kushughulikia mji wa Malakal ulioko kaskazini ambao kwa sehemu bado unadhibitiwa na waasi.

Lakini msemaji wa waasi alieleza kuwa wametoka tu Bor bila ya kupigana kufuatana na mikakati yao.


Brigedia Jenerali Lul Ruai Koang alisema waliondoka Bor kufuatana na amri ya viongozi wao wa siasa, ili kujitayarisha kwamalengo mengine.

Jeneral huyo alieleza kuwa Bor siyo muhimu tena, kwa sababu sasa ni magofu tu.

Pande zote mbili zinazoshiriki kwenye mazungumzo ya amani nchini Ethiopia zinasema zinakaribia kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano