WACHIMBAJI WA MIGODI WAGOMA A.KUSINI

Mgomo mkubwa zaidi wa wafanyakazi wa machimbo ya madini ya Platinum nchini Afrika Kusini, utaanza siku ya Alhamisi, kulalamikia mishahara duni.

Mgomo huo utasitisha uchimbaji wa madini hayo katika migodi ya kampuni tatu mikubwa zaidi duniani kwa uzalishaji wa madini ya Platinum.

Chama cha wafanyakazi wa sekta ya madini nchini humo AMCU kimesema kuwa zaidi ya wafanyakazi elfu sabini wataanza mgomo huo siku ya Alhamisi, hadi matakwa yao yatakapotimizwa.

Huu ni mgomo mkubwa zaidi kuwahi kutokea katika secta ya uchimbaji wa madini ya Platinum tangu mkasa wa mwaka juzi wa Marikana ambapo wachimba migodi wapatao 34 walipigwa risasi na polisi walipokuwa wakiandamana kuendeleza mgomo wao , uliotajwa na serikali kuwa haramu.


*MGOMO HALALI*

Safari hii gomo huu wa kudai nyongeza ya mishahara unaongozwa na AMCU chama cheye msimamo mkali cha kutetea wafanyaki wa migodini na mafundi katika sekta ya ujenzi.

Wachimba migodi hao ambao hufanya kazi kwenye machimbo ya kina kirefu sana, wanadai mishahara ya takriban dola elfu moja na mia mbili kwa mwezi, ikiwa ni maradufu ya mishahara wanayopokea sasa.

Tofauti na mgomo wa Marikana, mgomo huu wa sasa ni halali kisheria.

Kampuni zote tatu za Anglo American, Impala na Lonmin Platinum zimethibitisha kupokea notisi za mgomo.

Hata hivyo wanadai hawawezi kumudu kulipa nyongeza hiyo inayodaiwa kwa sababu ya gharama za uzalishaji ni kubwa namauzo ni haba.

Afrika Kusini ndio nchi inayozalisha madini ya Platinum kwa wingi zaidi huku asilimia 80% ya madini hayo yakiwa bado hayajachimbwa.