ANC WAKUMBWA NA KASHFA YA KUFUJA PESA ZA MAZISHI YA MANDELA

Upinzani nchini Afrika Kusini unataka uchunguzi kufanywa kuhusiana na madai ya ubadhirifu wa pesa zilizotengwa na chama hicho kwa matumizi wakati wa hafla ya mazishi ya hayati Nelson Mandela.

Matakwa hayo ya upinzani yametolewa baada ya taarifa za jarida moja kusema kuwa, sehemu ya dola elfu miatano zilizotengwa mahsusi kwa shughuli ya kuwasafirisha waombolezaji katika mazishi ya Mandela, zilitumiwa kwa shughuli nyinginezo ikiwemo kushonesha fulana za chama cha ANC.

Chama cha ANC ambacho kimezongwa na kashfa za ufisadi hakijajibu tuhuma hizo.

Duru kutoka mji wa East London zimesema takriban dola laki tano zilitengwa kando kusaidia katika kuwasafirisha waombolezaji wakati wa ibada maalum ya Nelson Mandela.

Hata hivyo fedha hizo zilielekewa kwa kampuni nyingine ambazo hazikua zikitoa huduma za uchukuzi.

Diwani mmoja wa chama cha Democratic Alliance ameambia BBC kwamba zilitolewa risiti bandia.

Manispa hio imesema inasubiri ripoti kamili kuwasilishwa mbele yake mwishoni mwa mwezi huu. Utawala wa Rais Jacob Zuma unakabiliwa na uchaguzi mgumu mwaka huu wakati ukikumbwa nasakata nyingi za ufisadi.