WAHUDUMU WA AFYA WAUAWA PAKISTANI

Watu waliojihami katika mji wa Karachi nchini Pakistan, wamewaua kwa kuwapiga risasi wahudumu watatu wa afya wakiwemo wanawake wawili waliokuwa wanatoa chanjo ya Polio.

Hili ni shambulizi la hivi karibuni likiwalenga wahudumu wa afya wanaotoa chanjo ya Polio au ugonjwa wa kupooza.

Walioshuhudia shambulio hilo walisema waliona watu waliokuwa wamejihami kwa bunduki wakiwa wanaendesha Pikipiki wakiwapiga risasi wahudumu wa afya waliokuwa wanatoa Chanjo hiyo kwa watoto wadogo.

Mwanamke mmoja alifariki papo hapo wakati mwingine alifariki akipelekwa hospitalini.

Shambulizi hilo ni pigo kubwa kwa juhudi za Pakistan kupambana na ugonjwa huo unaolemaza.

Kando na Afghanistan na Nigeria, Pakistan ni moja ya nchi ambako ugonjwa wa Polio ni janga kubwa.

Wapiganaji wa Taliban wanapinga chanjo ya ugonjwa wa kupooza nawamekiri kuwaua wafanyakazi waafya wanaotoa chanjo hiyo nchini Pakistan.