Tume hiyo imesema kuwa matamshi ya Bwana Raila ni hatari na kwamba yanaweza kuzua vurugu na hivyo kumtaka kuomba radhi mara moja.
Aidha tume hiyo imemtaka Raila kutoa ushahidi wa madai yake la sivyo atake msahama tume hiyo. ''Licha ya kuwa uchaguzi ni siasa, matamshi ya Raila ni siasa mbaya,'' ilisema taarifa ya tume hiyo.
Raila alitoa matamshi yake katika muhadhara wa wafuasi wake katika jimbo la Kisumu Magharibi mwa Kenya ambako anatoka.
Tume ya uchaguzi inahoji kwa nini Raila hakutoa malalamiko hayo kama ushahidi wake wakati wa kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mwaka jana badala ya kutoa matamshi mwaka mmoja baadaye.
Odinga aliwania uchaguzi kama Rais mwaka 2013 mwezi Machi ingawa alishindwa na punde baadaye aliwasilisha kesi katika mahakama kuu kupinga matokeo ya uchaguzi huo.
Odinga anasisitiza kuwa aliibiwa ushindi wake katika kile ambacho kimewaudhi washirika wa kisiasa wa Rais Kenyatta ambao wamekuwa wakimtaka akubali alishindwa.