WAASI HUKO CAR WASITISHA MAPIGANO MJINI BANGUI

Wapiganaji kutoka makundi hasimu, walikumbatiana katika mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bangui baada ya majeshi ya Ufaransa kuwasaidia kukubali kusitisha vita.

Wapiganaji walisalimisha silaha wilayani Bimbo baada ya siku kadhaa za mapigano makali, kati ya wapiganaji wa kiisilamu na waristo.

Mji huo ambao umekumbwa na ghasia hivi karibuni umetulia ingawa mapigano yangali yanaendelea katika baadhi ya sehemu za nchi hiyo.

Mazungumzo ya Amani yanatarajiwa kuanza Jumatatu kuhusu uchaguzi wa Rais mpya.

Michel Djotodia, aliyekuwa Rais wa mpito baada ya wapiganaji wa Seleka ambao ni watiifu kwake kuingia mamlakani kwa njia ya mapinduzi mwezi Machi, ameondoka nchini humo huku duru zikisema anatafuta hifadhi nchini Benin.

Watu 1,000 wameuawa na maelfu ya wengine kuachwa bila maakazi tangu vita vilipozuka nchini humo mwezi Disemba.

Ufaransa imepeleka wanajeshi 1,600 nchini humo kulinda amani, wakishirikiana na wanajeshi wengine 4,000 wa Muungano wa Afrika.

Umoja wa Mataifa umetoa nyo kali kuhusu hali mbaya ya kibinadamu nchini humo.