Kupanda kwa Tanzania katika nafasi hizo mbili ni kutokana na kufuzu kwa nusu fainali ya Kombe la Chalenji na kufungwa na wenyeji Kenya bao 1-0 katika mechi iliyokuwa na ushindani mkubwa.
Nchi 10 bora kwa mujibu wa takwimu hizo ni Hispania, Ujerumani, Argentina, Colombia, Ureno, Uruguay, Italia, Uswisi, Uholanzi na Brazil huku England ikiendelea kubaki katika nafasi ya 13.
Katika ukanda wa Afrika Mashariki, Uganda imeendelea kuongoza kwa ubora, lakini ikiteremka kwa nafasi moja 86 hadi 87.
Nchi nyingine za ukanda huo na viwango vyao vya ubora ni Kenya nafasi ya 109, Burundi 124 na Rwanda iliyopanda kwa nafasi tatu kutoka 134 hadi 130.
Katika bara la Afrika, Ivory Coast imeendelea kung'ang'ania kileleni ikikamata nafasi ya kwanza, huku ikishika nafasi ya 17 duniani. Kwa muda mrefu sasa Ivory Coast imekuwa ikiongoza viwango hivyo vya Fifa kwa upande wa Afrika.
Kwa upande mwingine, Misri imeibuka baada ya kupanda kwa nafasi 10 kutoka 41 hadi 31, wakati mabingwa watetezi wa Kombe la Mataifa ya Afrika, Nigeria imeporomoka kwa nafasi nne kutoka 41 hadi 45.
Hata hivyo mashabiki wa soka wa Nigeria wamekuwa wakiviponda viwango hivyo vya Fifa kwamba haviwatendei haki.
Wapinzani wa Tanzania katika mchezo wa kirafiki utaofanyika mwezi Machi, Namibia wenyewe wapo nafasi ya 125.