WAISRAEL WAOMBOLEZA KIFO CHA SHARON

Watu nchini Israel leo wanaanza kipindi kifupi cha maombolezi kufuatia kifo cha waziri mkuu wa zamani Ariel Sharon aliyefariki akiwa na umri wa miaka 85 baadaya miaka 8 ya kuwa hali mahututi.

Wananchi watatoa heshima zao zamwisho kwa mwili wake Jumapili kabla ya kuzikwa Jumatatu.

Viongozi wa dunia wametoa rambi rambi zao kwa Sharon, mtu aliyepigana katika vitaa vikuu vinne kabla ya kuingia katika ulingo wa siasa.

Lakini aliwaacha wapalestina wengi waliomuona kama adui wao wakiwa na hamaki.

Mkuu wa kituo cha afya cha Sheba mjini Tel Aviv alithibitisha kifo cha Sharon, Jumamosi mchana siku ya Sabato kwa wayahudi, zaidi ya wiki moja baada ya taarifa kutolewa kuhusuafya yake kuzorota.

Mmoja wa wanawe Sharon, Gilad Sharon, alisema kuwa babake amekwenda wakati alipoamua mwenyewe kwenda.

Rais wa Marekani Barack Obama na mkewe Michelle Obama, wamesema Sharon, alikuwa kiongozi aliyejitolea kuwahudumia watu wa Israel.

Rais Shimon Peres, mwandani mkuu wa Sharon japo alikuwa hasimu wake wa kisiasa aliyejiunga na serikali ya Muungano na Sharon mwaka 2001, alisema Sharon alikuwa mtu mwema aliyepigania watu wake na kuwapenda na kuwa watu pia walimpenda.

Wadhifa wa Sharon kama waziri mkuu ulifika kikomo baada ya kupatwa na kiharusi na kisha kuwa katika hali mahututi kwa miaka minane tangu mwaka 2006.

Wakati huu wote alikuwa anatumia mashine kupumua na mirija kulishwa chakula.

Kabla ya hali ya Sharon kuzorota aliongoza jeshi la Israel kuondoka katika ukanda wa Gaza ili kupunguza taharuki kati ya Israel na Palestina.