CCM YAONYA MAWAZIRI MZIGO NA WAFANYAKAZI

Chama tawala nchini CCM, kimeonya kwamba, hakitasita kuwachukulia hatua kali watendaji wa serikali wakiwemo mawaziri watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Kauli ya chama hicho imetolewa siku chache baada ya Rais wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete kulifanyia mabadiliko baraza lakela mawaziri huku baadhi ya mawaziri waliolalamikiwa na wananchi pamoja na wabunge kuwa ni mzigo kwa serikali wakiendelea kubakia katika nyadhifa zao.

Mara baada ya Rais Kikwete kutangaza mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, kuliibuka mjadala miongoni mwa wananchi, vyombo vya habari na wachambuzi wa masuala ya siasa kuhoji kulikoni Rais hakuchukua hatua ya kuwatimua mawaziri hao.

Hata hivyo, Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM, Bw. Nape Nnauye, amebainisha kuwa, haikuwa hoja ya chama hicho kuwafukuza mawaziri hao ila ametoa onyo kali kwao ikiwa hawatafanikisha majukumu na amza ya serikali kuwahudumia wananchi.

Mara kadhaa, maagizo ya kuchukuliwa hatua watendaji wa serikali wasiowajibika yamekuwa yakionekana kama kiini macho nawananchi wa kawaida.

Hata hivyo wachambuzi wa siasa walio na shaka na vitisho vya CCM kwa mawaziri mizigo, wanasema kuwa chama cha CCM ikiwa kitachukua hatua dhidi ya maafisa wake wasiotenda kazi vyema kitakuwa kinajiharibia sifa kama chama chenyewe.

Tuhuma dhidi ya baadhi ya mawaziri kupwaya katika utendajiwao zilitolewa na wananchi na kisha Wabunge wakati wa ziara yasiku 26 iliyofanywa na Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM kitaifa katika mikoa minne iliyoongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Bwana Abdulrahman Kinana, mwishoni mwa mwaka jana.

Disemba mwaka jana, CCM kupitia kikao chake cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa,ilimtupia mpira Rais Kikwete kuamua hatma ya mawaziri hao, huku kikifafanua kuwa, ilimshauri ama kuwafukuza, kuwahamisha wizara au kuwahimiza wafanya kazi.

Lakini katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais Kikwete hivi karibuni mawaziri hao waliendelea na nyadhifa zao