KAYA ZAIDI YA 500 ZAKOSA MAHALI PAKUISHI

Zaidi ya kaya 500 katika kijiji cha Magole wilaya ya kilosa mkoani morogoro hazina mahala pakuishi baada ya nyumba walizokuwa wakiishi kusombwa na mafuriko pamoja na mazao na mifugo yao kutokana na mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia leo.


Wakizungumza na star tv wakazi wa kijiji hicho wamesema mvua hizo zimeleta madhara makubwa kwa upande wao kwani mpaka sasa hawajapata misaada yoyote ya kibinadamu na hawajui wapi pakuelekea.

Kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali hapa nchini tayari zimeleta madhara kwa wakazi zaidi ya 2500 mkoani morogoro baada ya kusababisha mafuriko yaliyobomoa nyumba na kusomba mazao, chakula pamoja na mifugo Wakizungumza kwa masikitiko kwa kutojua nini hatima yao, wakazi wa kijiji cha Magole wameiomba serikali kupeleka misaada ya kibinadamu ili kunusuru maisha yao.

Mkuu wa mkoa wa morogoro amefika eneo la tukio na kuwaomba wananchi kuwa watulivu wakati serikali ikijipanga kutoa misaada kwa wahanga wa mafuriko hayo.

Aidha mbali na mafuriko hayo kuleta madhara kwa wakazi hao pia zaidi ya abiria 2000 wamekwama njiani kwa zaidi ya masaa matano kutokana na mafuriko hayo kuvunja daraja la magole barabara ya morogoro dodoma hivyo wasafiri hao kushindwa kuendelea na safari yao.

Mpaka star tv inaondoka eneo la tukio juhudi za uokoaji zilikuwa zikiendelea huku helkopta ya jeshi la polisi ikiwasili kwa ajiri ya kutoa msaada kwa wale walionasa kwenye maeneo hayo.

Chanzo: StarTv