"Rais Kikwete amesikitishwa kwa uongo huu na ametoa ushauri kwa wahariri wa gazeti hili, kuacha kutunga madai yasiyo na ukweli, ambayo yanaweza kujenga chuki na kuchanganya watu wa nchi hizi jirani na rafiki.
"Wakati huu ambao Rais Kikwete na Rais Paul Kagame wa Rwanda, walishakubaliana kuimarisha uhusiano wa kirafiki baina yao na nchi hizi mbili mjini Kampala, Uganda, gazeti hilo linachofanya ni kuweka mazingira magumu ya nia hiyo njema na Rais Kikwete angependa kujua wahariri hao wana lengo gani," alieleza Balozi Mwaipaja.
Balozi alionya kuwa Ubalozi wa Tanzania hautachukulia habari hiyo kirahisi, hasa kwa kuzingatia kuwa gazeti hilo limesambazwa katika vitongoji vyote vya Rwanda.
Tuhuma Kwa mujibu wa taarifa ya Balozi Mwaipaja, gazeti hilo limedai kuwa muasisi wa chama cha Rwanda National Congress (RNC), aliyetajwa kwa jina moja la Dk Rudasingwa, mshauri wa chamahicho, Condo Gervais na makamanda wa ngazi za juu wa kikundi cha waasi nchini humo cha FDLR, Luteni Kanali Wilson Irategeka na Kanali Hamadi, walikuwa Tanzania mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mbali na kuwa nchini, gazeti hilo lilidai kufanyika mkutano kati ya Rais Kikwete na viongozi hao wa waasi katika makazi rasmi ya Rais.
Gazeti hilo lilidai pia kuwa Waziri Mkuu wa zamani wa Rwanda, Faustin Twagiramungu, alikuwa nchini na alikutana na wawakilishi hao wa RNC na FDLR, Dar es Salaam.
Madai mengine yalihusisha Idara ya Uhamiaji ya Tanzania, kwamba ilitoa hati za kusafiria za Tanzania kwa waasi hao ambazo walizitumia kusafiri katika nchi mbalimbali ikiwamo Msumbiji Desemba 20 mwaka jana. Pia kwamba kuna taasisi imeanzishwa nchini ambayo kazi yake ni kupanga na kusaidia safari za wapiganaji wa FDLR.
Akifafanua hoja moja baada ya nyingine katika taarifa hiyo iliyosambazwa pia kwa vyombo vya habari nchini humo, Balozi Mwaipaja alianza na madai ya mkutano wa Rais Kikwete na waasi hao.
"Hakukuwa na mkutano kama huo katika makazi rasmi ya Rais Kikwete Dar es Salaam wala Dodoma au kokote, tena Rais Kikwete hajawahi kukutana na ofisa yeyote kati ya waliotajwa mahali kokote ndani na nje ya Tanzania.
"Mbaya zaidi, siku ambayo gazeti la News of Rwanda linadai kuwa mkutano huo ulifanyika, Alhamisi Januari 23, Rais Kikwete hakuwa nchini, bali alikuwa Davos, Uswisi akihudhuria Mkutano wa Uchumi wa Dunia (WEF)," alieleza Balozi Mwaipaja.
Balozi alieleza pia kuwa muasisi waRNC na mshauri wake na makamanda wa FDLR, hawakuwa nchini wiki iliyopita na rekodi za Uhamiaji zimethibitisha kuwa hawajawahi kufika nchini katika miaka ya hivi karibuni.
Kuhusu taarifa za Twagiramungu kuwa nchini wiki iliyopita, Balozi Mwaipaja alisema kiongozi huyo hakuwapo wala hakuwa na mkutano wowote na waasi wenzake na zaidi, kumbukumbu za Uhamiaji zinathibitisha kuwa hakuingia wala kutoka nchini.
Balozi Mwaipaja pia alisikitika na madai kuwa Uhamiaji ilitoa hati za kusafiria kwa Wanyarwanda hao na kufafanua kuwa kitu kama hicho hakijafanyika kwa raia wa Rwanda.
"Si kazi ya Tanzania kutoa hati za kusafiria kwa raia wa nchi zingine, "alifafanua.
Kuhusu madai ya kuanzishwa kwa taasisi ya kusaidia waasi, Balozi Mwaipaja alisema gazeti hilo, linapaswa kujua walipo wapiganaji hao na mahali wanakofanyia kazi.
"Taarifa hizi kwa kweli ni uongo wa hatari uliotungwa na wahariri wa gazeti hili na lengo lao baya na la wazi la kumshambulia Rais wa nchi rafiki na kujaribu kuaminisha umma kuwa Tanzania inashirikiana na maadui wanaopingana na Serikali ya Rwanda," alieleza Balozi huyo.
Aliokutana nao siku (Januari 23) ambayo gazeti hilo linadai Rais Kikwete alikutana na waasi Dar es Salaam, alikutana katika Hoteli ya Sheraton jijini Davos na Naibu Waziri Mkuu wa Uingereza, Niuck Clegg na kisha kukutana na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Jetro ya Japan. Rais pia siku hiyo alikutana nakufanya mazungumzo na Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), Rajiv Shah.
Baada ya hapo, Rais alishiriki mijadala na mikutano katika Hoteliya Derby jijini hapo, ambayo ilihusu masuala mbalimbali ya uchumi.
Chokochoko hizi zinatokea baada ya majeshi ya ulinzi ya Tanzania kushiriki kupambana na kukisambaratisha kikundi cha waasicha M23 kilichokuwa kikiendesha hujuma zake dhidi ya Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Mashariki mwa nchi hiyo. Kikundi hicho kilikuwa kinadaiwa kuhusishwa na Serikali ya Rwanda.