ZITTO NIKO TAYARI

LICHA ya uongozi wa Chadema kutaka wanachama wa chama hicho kuacha kumpa ushirikiano Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, yeye amesema yuko tayari kufanya kazi na kiongozi yeyote wa chama hicho aliye tayari.

"Mimi niko tayari kufanya kazi na kiongozi yeyote wa Chadema ambaye atakuwa tayari kufanya kazinami, kwa sababu naamini suala hapa ni ujenzi wa nchi yetu, ni ujenzi wa Taifa letu na naamini hatakama nina mawazo kidogo, lakini ni kwa ajili ya kuiendeleza nchi yetu," amesema Zitto.

Akihojiwa jana na mtandao wa kijamii wa millardayo.com, Zitto alisema sasa hivi kuna masuala makubwa kuhusu Katiba ya nchi na angependa wananchi wajielekeze huko.

"Sijafurahishwa sana na kinachoendelea hivi sasa, maana yake wananchi wameacha kujadili masuala ya msingi yanayowahusu, nasikitika kuona vyombo vya habari ni habari za Zitto na Chadema, nashukuru jambo hili limekwisha sasa kwa muda huu," alisema akimaanisha mgogoro na chama chake.

Alisisitiza kuwa bado ni mwanachama wa Chadema, licha ya Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Wilbrod Slaa, kutoa amri ya watu kumnyima ushirikiano "lakini pale nitakapohitajika nitafanya shughuli za Chadema, nitafanya shughuli za nchi yangu.

"Kuhusu ushindi wake wa juzi mahakamani, alisema si ushindi dhidi ya chama, kwa sababu hawezi kushindana na chama chake, kwa kuwa kimemlea na amekitumikia kwa muda wote, zaidi ya nusu ya umri wake."Kwa hiyo salamu ambazo napenda wananchi wazifahamu ni kwamba tunahitaji kuheshimu sana demokrasia na misingi ya haki za binadamu," alisema.

Akizungumzia uamuzi wa Mahakama, uliotolewa na Jaji John Utamwa, alisema utaweka utaratibu kwamba watu ambao ni wanachamawa vyama hawataonewa, hawata dhulumiwa wala kukandamizwa na watakuwa huru kutoa maoni yao wanapohitaji kufanya hivyo.

"Nataka niseme wazi kabisa kwa Watanzania ambao ni wanachama wa vyama vingine, wasio na vyama na kwa wana Chadema, ushindi huu si dhidi ya Chadema, ni wa Watanzania wote wanaopenda siasa safi na taratibu za utawala bora zifuatwe kwenye taasisi zetu."Ni ushindi dhidi ya wanaotaka kukandamiza demokrasia ndani ya vyama, ni ushindi dhidi ya wahafidhina wasiotaka mabadiliko katika vyama," alisema.

Lissu Akizungumza muda mfupi baada ya hukumu hiyo juzi, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema suala ambalo Chadema inalisema kuwa muhimu ni kwa wanachama wake kuhakikisha hawampi nafasi Zitto lakini kama atataka kuandaa mikutano kwa jina lake anaweza kuendelea, kwa kuwa kwa mujibu wa Mahakama bado mwanachama wa Chadema.

Hata hivyo alisisitiza kuwa Zitto ni mbunge wa Mahakama na kwamba 'ubunge wa Mahakama' una mwisho wake, kama mbunge wa Mahakama atapokea posho, atapokea mishahara atakwenda safari za PAC kwa hiyo ana haki zote kama mbunge.

"Kwenye vikao kama ni mwanachama kwenye tawi lake atashiriki, lakini kwenye vikao vingine vya chama ambavyo si mwanachama na si mjumbe hatashiriki," alisema Lissu.

Alisema kambi rasmi ya upinzani ina taratibu zake na moja ya taratibu ni kwamba kama mjumbe wa kambi haendani na matakwa ya kambi, moja ya adhabu ni kuzuiwa kuingia kwenye vikao.

"Zitto anaweza kuzungumzia masuala ya chama mahali popote. Amri ya Mahakama inasema KamatiKuu au chombo kingine cha chama kisizungumzie wala kuamua uanachama wake … haijamziba mdomo kuzungumza masuala ya chama kama ambavyo mimi nawezakuzungumzia mambo ya chama," alisema Mwanasheria huyo.

Pamoja na pingamizi la muda alilopewa Zitto na Mahakama Kuu, kisheria hudumu kwa miezi sita, lakini kuna uwezekano wa mbunge huyo kumaliza ubunge wake kwa kutumia amri hiyo ya Mahakama.

Baadhi ya wanasheria waliozungumza na gazeti hili jana, walisema licha ya sheria ya sasa kusisitiza kuwa pingamizi la muda lidumu kwa miezi sita, lakini iwapo kesi yake ya msingi ambayo imefunguliwa mahakamani itakuwa haijaisha, mbunge huyo anaweza kuomba kuongezwa pingamizi hilo kwa miezi sita mingine.

"Kisheria pingamizi hili linaweza kudumu kwa mwaka mmoja, yaani kwa vipindi viwili tofauti," alisema mwanasheria maarufu Alex Mgongolwa.

Mgongolwa na Mkurugenzi wa Kituocha Haki za Binadamu, Hellen Kijo-Bisimba wote walikubali kuwa mbunge huyo anaweza kumaliza muda wake wa ubunge chini ya amri ya Mahakama iwapo ataendelea kuomba zuio la muda, kutokana na hali itakavyokuwa ndani ya chama chake.

Mgongolwa Mgongolwa akifafanua jambo hilo, alisema mwaka mmoja wa pingamizi hilo ukiisha, ni wazi kuwa kama Chadema itakuwa bado inahitaji kumhoji ni wazi kuwa itamwandikia barua yenye tarehe ya wakati huo."Kisheria hilo ni jambo jipya, hivyo mlalamikaji anaweza kwenda tena mahakamani kuomba zuio lingine lamuda kwa jambo ambalo anaitiwa na chama chake kama jambo jipya,"alisema.


"Kwa macho ya haraka unaweza kudhani pingamizi mwisho wake ni mwaka mmoja, lakini sisi tunaotafsiri sheria, tunaona pingamizi la Mahakama linaweza kudumu hata miaka mitatu … ukitaka kuamini angalia suala la Hamad Rashid Mohamed wa CUF amemaliza miaka miwili sasa chini ya zuio la Mahakama," alisema Mgongolwa. Lakini alisema utoaji amri hiyo ya zuio la muda ni utashi wa Mahakama itakavyoona kwa hali ilivyo wakati huo. Lakini pia amri hiyo inatolewa tu iwapo mlalamikaji ataomba, na Mahakama inaweza kumpa tuzo hiyo au kumnyima.

Bisimba Katika ufafanuzi wake, Bisimba alisema Zitto anaweza kuendelea kupumua kwa nguvu za Mahakama iwapo atakuwa na hoja ambazo zitaishawishi kuendelea kumpa tuzo hiyo ya zuio la muda.

Alisema kesi ya msingi ambayo iko Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kama itakuwa haijaisha kusikilizwa, miezi sita ya awali ikimalizika, Zitto ana haki ya kuomba miezi mingine sita; lakini awe na hoja ya msingi ambayo itaishawishi Mahakama.

"Mahakama inaweza kukataa kama itaona hakuna hoja za msingi na kama mazingira ya kufunguliwa kwakesi hiyo yatakuwa yamebadilika," alisema mwanasheria huyo.

Anguko Bisimba katika mazungumzo yake alisema siasa ni mchezo mchafu na vyama vya upinzani vimekuwa vinavurugika na kusambaratika hasaunapokaribia uchaguzi mkuu.

"Yaliyotokea NCCR-Mageuzi na TLP haikuwa bahati mbaya, vyama hivi vilipata kuwa na nguvu; lakini vilidhoofu na haya yanayoendelea ndani ya Chadema si bahati mbaya,"alisema Bisimba.

Alisema chama cha upinzani ambacho angalau Watanzania waliona kina nguvu ni Chadema, lakini anashangaa chama hicho sasa kinapita kwenye nyayo za vyama vingine ambavyo vilianguka.

Chanzo: Habari leo