PAPA AFUKUZA KAZI MAKADINALI

MAKADINALI wote isipokuwa mmoja waliokuwa wakisimamia benki ya Vatican wamefutwa kazi na Papa Francis. Waliokumbwa na 'fagio hilo la chuma' ni makadinali wanne ambao ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Kadinali Tarcisio Bertone SDB,Kadinali Odilo Scherer kutoka Brazil, Telesphore Toppo kutoka India na Domenico Calcagno kutoka Vatican.Kadinali Jean-Louis Tauran ambayeni Mkuu wa Baraza la Upapa linalohusika na Mijadala ya Kidini, amenusurika kwa mujibu wa gazetila kila wiki la Kikatoliki la The Tablet.

Gazeti hilo lilieleza jana kuwa isipokuwa Calcagno, makadinali hao wote ndio kwanza walikuwa wametimiza miezi 11 tangu wateuliwe katika kipindi cha pili cha miaka mitano, wakiwa wameteuliwa na Papa Benedict XVI muda mfupi kabla ya kujiuzulu.

Benki hiyo ya Vatican ilikumbwa nakashfa ya utakatishaji fedha mwaka2010 baada ya waendesha mashitaka wa Italia kugundua shughuli zenye shaka zihusuzo fedha chafu ndani ya benki.

Mwenyekiti wa Benki hiyo, Ettore Gotti Tedeschi na naibu wake, Paolo Cipriani walichunguzwa baada ya polisi kukamata euro milioni 23 kutoka kwenye akaunti ya benki hiyo.

Ilidaiwa kuwa ingawa benki hiyo ilikuwa inadai kupambana na utakatishaji fedha, ilivunja sheria kwa kujaribu kuhamisha fedha hizobila kutambulisha mtumaji wala mpokeaji, au zilikuwa zinatumika kwa shughuli gani.


Tuhuma hizo zilikanushwa kwa nguvu zote na Vatican. Papa Francisameteua makadinali wengine kuziba nafasi za aliowatimua na kuunda alichokiita Tume ya Makadinali ya Kusimamia Taasisi kwa ajili ya Kazi ya Dini (IOR), ambao ni makadinali Christoph Schönborn (Vienna), Thomas Collins (Toronto); Santos Abril y Castillo´ (St Mary Major) na Kadinali Pietro Parolin (Waziri wa Mambo ya Nje).

Wajumbe wa Tume hiyo watachagua rais katika siku chache zijazo itakapofanya mkutano wake wa kwanza. Kadinali Bertone ndiye alikuwa Rais hadi alipoondolewa.

Kadinali Jorge Mario Bergoglio, ambaye alipewa jina la Papa Francis, ni Papa wa kwanza Muargentina na wa kwanza kutoka nje ya Ulaya kwa zaidi ya miaka 1,000 baada ya kuchaguliwa Machi 13 mwaka jana.

Papa Francis anaweza kuwa haoneshi mapenzi mengi kwa makadinali wake wa benki, lakini anajihusisha zaidi na wanandoa, kwani ametuma mialiko kwao kwa ajili ya kusherehekea Siku ya Wapendanao pamoja naye.

Kadi iliyoandikwa 'Furaha ya Ndiyo Daima' ilitolewa na Vatican ikiwaalika wanandoa wasio wa jinsia moja kukaa faragha na Papa mwezi ujao.

Kwa hafla hiyo iliyoandaliwa na Baraza la Upapa la Vatican kwa Familia, washiriki wametakiwa kujiandikisha ifikapo Januari 30 ili kupata nafasi ya kukaa.