SUDANI KUSINI NA WAASI WAKUBALIANA KUMALIZA VITA

Waakilishi wa serikali ya Sudan Kusini wanasema kuwa serikali imetia saini mkataba wa kusitisha vita na waasi.

Kulingana na mkataba huo uliotiwa saini mjini Addisa Ababa Ethiopia, mapiganao yanapaswa kusitishwa katika muda wa masaa 24.

Aidha mkataba huo unatarajiwa kusitisha vita vya mwezi mmoja vilivyoanza tarehe 15 Disemba mwaka jana kati ya waasi na serikali.

Mazungumzo ya amani yamekuwa yakikumbwa na matatizo kuhusu swala la wafungwa 11 wa kisiasa ambao bwana Riek Machar anayeongoza waasi alitaka waachiliwe kama sharti la kutia saini mkataba wa amani.

Wiki jana wanajeshi wa serikali walifanikiwa kukomboa miji kadhaa iliyokuwa imetekwa na waasi.

Zaidi ya watu 500,000 wamelazimika kutoroka makwao kutokana na vurugu hizo za mwezi mmoja.