MJI WA BOR WAHARIBIWA VIBAYA

Habari kutoka Sudan Kusini zinasema kuwa mji wa Bor uliokombolewa hivi karibuni na wanajeshi wa Serikari umeharibika kabisa kufuatia mapambano na waasi.

Mwandishi wa BBC aliyetembelea Bor siku moja baada ya mji huo kukombolewa amesema kwa wakati huu hakuna mtu yeyote ndani ya mji huo.

Nyumba zimeteketezwa na Soko Kuu limeharibiwa kabisa.

Maiti zilizoteketea zilionekana kila mahali nje ya hospitali ambayo ilionekana kuporwa.

Wagonjwa walisema kuwa kuna watu waliopigwa risasi ovyo na kuuawa.

Wajumbe kutoka pande zote mbili wanatarajiwa kuanza mashauriano katika mji mkuu wa Ethiopia wakati wowote kuanzia sasa.

Wakati huohuo, wanajeshi wa Sudan Kusini walipambana na waasi Jumatatu huku Umoja wa Mataifa ukisema kuwa wanajeshi walijaribu kuingia kwa nguvu katika kambi yake inayo wahifadhi maelfu ya wakimbizi wa ndani waliotoroka vita.

Maelfu ya raia wasio na hatia wameuawa na karibu nusu milioni kuachwa bila makao huku katika vita hivyo ambavyo vimeingia sasa wiki ya sita.

Mazungumzo ya amni kuhusu mzozo huo nayo yamekwama nchini Ethiopia.

Umoja wa Mataifa umesema kuwa uhalifu dhidi ya binadamu umefanywa na pande zote kwenye mgogoro huo.