WATUMISHI 1,360 WAKUTWA NA VYETI FEKI

UDANGANYIFU katika vyeti wakati wa kuomba ajira umeendelea kukithiri nchini, ambapo ndani ya mwaka mmoja tu, kuanzia Julai mwaka jana mpaka Juni mwaka huu, watumishi 1,360 wamekutwa na vyeti visivyo halali. Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde, alisema hayo jana mbele ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk ShukuruKawambwa, wakati wa uzinduzi wa bodi mpya ya baraza hilo.

Katika uhakiki huo, baadhi ya watumishi wakiwemo wa Serikali walikutwa wakitumia vyeti vya kughushi ambavyo imebadilishwa matokeo, wengine walikutwa na vyeti vyabandia huku wengine wakitumia vyeti vya watu wengine.

Hii si mara ya kwanza kwa Serikali kuelezea uozo huo katika elimu, ambapo Julai mwaka jana Msemaji wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Riziki Abraham, alitoa taarifa ikielezakuwa Sekretarieti hiyo ilibaini kuwepo kwa udanganyifu wa vyeti 677, kwa watumishi serikalini.

Aidha, Oktoba mwaka jana Ofisa Habari na Mawasiliano waOfisi ya Sekretarieti hiyo, Kasim Nyaki, alieleza kuwa vyeti vya Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi (Veta) ni miongoni vyeti vinavyoongoza kutumiwa katika udanganyifu kwa watu wanaoomba kazi kupitia Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

Nyaki alisema kuwa kati ya watu 517 waliotumia vyeti vya Veta kuomba ajira kupitia sekretarieti hiyo, watu 304 walitoa vyeti halali, lakini watu 213 walighushi.

Mbali na hao, alikwenda mbali zaidi na kueleza kuwa kati ya watu 13,554 walioomba ajira katika miaka mitatu yaani 2010, 2011 na 2012, watu 816 walibainika kudanganya kwa kutumia vyeti vya taasisi mbalimbali za elimu, vyeti vya kuzaliwa na vinginevyo.

Kutokana na hali hiyo, Dk Msonde alisema Baraza hilo limeamua kushirikiana kwa karibu na mamlaka za ajira na udahili, ili kuhakikisha uhakiki wa vyeti vinavyotolewa na baraza hilo, unafanyika kabla ya mtahiniwa kuajiriwa au kudahiliwa.

Mbali na ushirikiano huo, Baraza hilo limeazimia kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya kutumia udanganyifu katika vyeti.

Aidha, Baraza hilo pia limeanzakutoa vyeti vyenye picha ya mmiliki kuanzia 2008, ili kupunguza kasi ya udanganyifu huo.

Katika hatua nyingine, Baraza hilo limeanza utaratibu wa kutoa vyeti mbadala kwa watahiniwa waliopoteza vyeti vyao kwa waliohitimu kuanzia mwaka 2008 ambao vyeti vyao vilikuwa na picha.

Dk Msonde alisema hatua hiyo ya kutoa vyeti kwa waliopoteza,inatarajiwa kupunguza changamoto zilizokuwa zikiwakabili watahiniwa waliopoteza vyeti vyao kwa sababu mbalimbali kwa kupata vyeti mbadala, huku likiweka utaratibu madhubuti kuhakikisha fursa hiyo haitumiwi vibaya.

Akizungumzia kudhibiti wizi na udanganyifu katika mitihani, alisema Baraza kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wamedhibiti na kuondoa kabisa tatizo la wizi wa mitihani ya taifa na kwa kiasi kikubwa na kudhibiti udanganyifu wakati wa ufanyaji mitihani.

Alisema Baraza hilo linakabiliwa na upungufu wa fedha za kuendesha mitihani yataifa, ambao usipofanyiwa kazi,utaathiri uendeshaji wa mitihani ya kidato cha sita na ualimu.

Ukata huo alisema pia utaathiriuongezaji wa viwango vya posho za wasahihishaji kwa mitihani ya kidato cha nne, sitana mitihani ya ualimu kama ilivyokuwa imepangwa.

Alisema katika mwaka wa fedha 2014/15, kulikuwa na umuhimu wa kuongeza posho ya wasahihishaji kwa kuwa posho hiyo imekuwa ikilalamikiwa na washiriki kwa kuwa ni ndogo ikilinganishwa na posho zinazolipwa na mamlaka nyingine, ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa shughuli za mitihani.

Akizindua bodi hiyo, Waziri Kawambwa alisema wakati matokeo ya kidato cha nne mwaka huu yakianza kutolewa kwa mfumo mpya wa Wastani wa Pointi (GPA) ni vema kutoa elimu wakati huu kabla na baada ya mtihani, ili kuzuia mtafaruku.

Alisema utoaji wa elimu kwa wadau wote wa elimu, wanafunzi na wazazi utasaidia kudhibiti upotoshaji mara utekelezaji utakapoanza.

“Hili lifanywe kwa juhudi na umakini ili kuepusha upotoshaji unaoweza kufanywa na baadhi ya watu, elimu kuhusu mfumo mpya wa kutunuku matokeo itolewe kwa kutumia aina zote za mawasiliano na umma kabla, wakati na baada ya mitihani.

Bodi hiyo mpya inaongozwa na Mwenyekiti wake, Rwekaza Mukandala na wengine ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Taaluma), Profesa Makenya Mabhoko, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Watoto, Benedict Misani na Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule Binafsi, Mahmoud Mringo.

Wengine ni Mkurugenzi wa Baraza la Mitihani la Zanzibar, Ameir Selemani Haji, Mkuu wa Skuli ya Ualimu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar, Dk Maryam Jaffar Ismail, Mkurugenzi wa Idara ya Sekondari, Asia Iddi Issa, Mwakilishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Shaban Kamchacho, Mkuu wa Sekondari ya Kisimiri Meru, Emmanuel Kasongo na Mwalimu Mkuu Shule ya MsingiKimara Baruti, Rehema Ramole.