BOTI YAZAMA, YAUA WATATU MAHARUSI WAOKOLEWA

WATU watatu wamekufa na wengine zaidi ya 70 wameokolewa wakiwemo bwana na bibi harusi ambao walitoka kufunga ndoa muda mfupi kabla ya tukio hilo kufuatia boti waliyokuwa wakisafiria kugonga mwamba na kuzama ndani ya Ziwa Tanganyika.

Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali ambazo zimethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Jafari Mohammed zinaeleza kuwa tukio hilo lilitokea juzi katika Kijiji cha Kalalangabo Wilaya ya Kigoma mkoani Kigoma.Akielezea tukio hilo, Kamanda Mohammed amesema kuwa hadi sasa haijafahamika ni watu wangapiwalikuwa wamepanda kwenye boti hiyo kwani haikuwa imesafiri katika taratibu za kawaida ambazo zinasimamiwa na Mamlaka ya usalama wa nchi kavu na majini (SUMATRA).

Kamanda huyo wa Polisi alisema kuwa vikosi vya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kushirikiana na wavuvi waliowahi kufika katika eneo hilo walifanikiwa kuokoa watu 20 ambao walikimbizwa Hospitali ya Mkoa Kigoma ya Maweni kwa matibabu na wengine inawezekanawalikimbia ili kupoteza ushahidi waidadi ya abiria waliokuwa kwenye boti hiyo.

Kwa upande wake Mganga wa Zamu katika Hospitali ya Mkoa Kigoma Maweni, Haika Masula amethibitisha kupokelewa kwa miili mitatu ya watu waliofariki kwenye tukio ambapo mmoja ametambuliwa kwa jina la Salama Juakali huku maiti wawili watoto wakiwa hawajatambuliwa hadi sasa.

Masula alisema kuwa katika idadi ya majeruhi waliopokelewa hospitalini hapo hadi kufikia jana mchana watu 11 waliruhusiwa kurudi nyumbani baada ya kupatiwa matibabu na hali zao kurejea katika hali ya kawaida.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Wavuvi kwenye Mwalo wa Kibirizi mjini Kigoma, Sendwe Ibrahim alisema kuwa walipokea taarifa za kuwepo kwa ajali ya boti juzi kuanzia majiraya saa tisa mchana na boti zikaanzakuelekea eneo la tukio kwa ajili ya kutoa msaada.Mwenyekiti huyo alisema kuwa hiyo haikuwa boti ya kubeba abiria ilikuwa ni boti ya uvuvi ambayo kwa idadi inayopaswa kubeba haipaswi kuzidisha abiria 20 na ndiyo maana boti hiyo ilipandisha watu kinyemela katika Kijiji cha Kalalangabo badala ya bandari ndogo ya Kibirizi mjini Kigoma.

Ajali hiyo imetokea wakati ShaabanHussein na Mariam Juma (18) wakazi wa Kijiji cha Mtanga wakitoka kufunga ndoa kwenye Kijiji cha Mwandiga Kigoma vijijini nyumbani kwa bibi harusini na ambapo hali za maharusi hao ambao walikuwemo ndani ya boti wakisindikizwa na ndugu na jamaa zao zinaendelea vizuri.Bwana harusi aliruhusiwa kutoka hospitalini hapo jana asubuhi wakati hali ya bibi harusi ikiendelea vizuri huku akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitaliya Maweni.



Chanzo: Habari Leo