Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa TAHLISO, Musa Mdede, alisema kumekuwa na utaratibu mbovu wa vyuo binafsi kupandisha ada, jambo ambalo linawanyima fursa masikini kupata elimu.
Mdede, alivitaja vyuo ambavyo vimeongezaada kuwa ni KCMC Moshi, Bugando Mwanza na St Francis kutoka sh milioni 2 zaawali hadi milioni 5 kwa mwaka.
"Kuna baadhi ya vyuo kama KCMC, kimezuia wanafunzi kuingia chuoni hadi waoneshe stakabadhi inayoonyesha kuwa amelipa ada mpya, japokuwa TCU imekwisha waandikia barua wasitishe ongezeko hilo kwa mwaka wa masomo 2014/15," alisema Mdede.
Aliongezea kuwa asilimia 50 ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na vyuo vikuu nchini kwa mwaka wa masomo 2014/15, watakosa mikopo japokuwa wana sifa ya kukopeshwa.
Mdede, alisema ili kumsaidia kila mtanzania kupata elimu ni vyema serikali ikatoa mikopo kuanzia ngazi ya cheti na stashahada kwa wanafunzi wote wenye sifa.
"Tumefurahi kuona kwa mara ya kwanza nchini, Chuo Kikuu cha Dodoma kuna baadhi ya wanafunzi ngazi ya stashahada wamepewa mikopo, kwa mfano huo serikali ijipange kuwapa mikopo ili tuweze kuwa na taifa la wasomi," alisema Mdede na kuongeza.
Pia, kutokana na kupanda kwa gharama za maisha, serikali inatakiwa kuwapandishia fedha za kujikimu kutoka sh7,500 ya sasa hadi 15,000 kwa siku.