VIJANA WANASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI KWA KULAWITI WANAFUNZI

VIJANA wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro kwa tuhuma za kuwalawiti wanafunzi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Koka Moita, alisema tukio hilo lilitokea Oktoba Mosi, mwaka huu katika Kijiji cha Longuo B, Tarafa ya Moshi Magharibi wilayani Moshi.

Moita alisema wanafunzi waliolawitiwa mmoja wa miaka 10 na wengine wana miaka kati ya 12 na 13. Aliwataja vijana waliofanya kitendo hicho ni Musa Selemani (13) na Daudi Raphael (15).

Alisema chanzo cha tukio ni wakati watoto hao walipokuwa wakielekea shuleni, walipofika njiani watuhumiwa waliwaita pembeni ya kichaka watoto hao, na kuwafanyia kitendo hicho cha kinyama kwa nguvu.

Kutokana na kitendo hicho, wanafunzi hao walipelekwa Hospitali ya Rufaa KCMC kwa matibabu zaidi na wanaendelea vizuri, huku watuhumiwa wakishikiliwa na Jeshi la Polisi na uchunguzi zaidi unaendelea.