Mahabusu Daniel Alfred katika kituo cha Polisi Urafiki, eneo la
Ubungo, amefariki dunia kwa madai ya kupigwa na baadhi ya askari wa
kituo hicho.
Alfred aliyekuwa mkazi wa Sinza jijini hapa,
alifikishwa kituoni hapo kwa kosa la wizi wa kuaminiwa na kuwekwa
mahabusu wakati akisubiri kufikishwa mahakamani juzi(Jumatatu) ili
kusomewa mashitaka yake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius
Wambura jana alithibitisha kutokea kwa kifo hicho, huku akisema kijana
huyo alikuwa akifanya fujo na kuwapiga wenzake wakati akiwa chumba cha
mahabusu.
Kamanda Wambura alisema kuwa baada ya kifo chake waliupeleka mwili wake hospitali.
Wambura alisema ripoti ya daktari baada ya uchunguzi, ilionyesha kwamba mahabusi huyo alikuwa mgonjwa.
Shuhuda ambaye hakutaka jina lake litajwe
gazetini, alisema alikwenda kituo hapo kumuona ndugu yake lakini alikuta
askari wakimpiga.
“Mimi sijui kama alikuwa na matatizo ya kiafya,
lakini niliona akipigwa sana na askari wa kituo hicho...yaani
inasikitisha sana, jamaa alipigwa kama mpira wa gombania goli, mimi
nilikuwa najua kituo cha polisi ndiko usalama wa watuhumiwa unapatikana
kumbe hapana ndiyo maana nikaja kuwaeleza nilichokiona,” alisema mtoa
habari huyo.
Alisema hata kama kijana huyo alikuwa mgonjwa, anaimani kuwa aliuawa na polisi kwa kipigo kikali.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi