RAIS KENYATTA ATAKIWA THE HAGUE

Majaji wa mahakama ya jinai ya ICC wameamua kuwa rais wa Kenya hana budi ila kufika mahakamani binafsi Oktoba tarehe 8.

Majaji hao wamekatalia mbali ombi la mawakili wa rais Uhuru Kenyatta la kutaka aruhusiwe kuhudhuria kikao hicho kupitia kwa njia ya Video ama kikao hicho cha ana kwa ana kiahirishwe hadi siku nyingine kwani alikuwa amekabwa na kazi na majukumu kama rais wa Kenya.

Majaji hao wanasema kuwa Rais Uhuru Kenyatta hakutoa sababu madhubuti ya kukosa kuhudhuria kikao hicho maalum.

Majaji hao aidha wanasema kuwa Bwana Kenyatta lazima awe hapo ilikujibu maswali muhumi kuhusu ushirikiano wa serikali yake na kujadili maswala muhimu yatakayo jadiliwa katika kikao hicho.

Kenyatta alikuwa ameiamboa mahakama kuwa ameratibiwa kuhudhuria sherehe za kuadhimisha uhuru wa Uganda.

Kauli hiyo inawadia wakati ambapo mwendesha mashataka wa mahakama hiyo Fatou Bensouda alikuwa amepinga ombi la rais Kenyatta la kuahirisha kikao hicho ama kuruhusiwa kushiriki kikao hicho kwa njia ya video.

Bi Bensouda alikuwa ameilalamikia mahakama hiyo akidai kukosa ushahidi wa kutosha baada ya serikali ya Bw Kenyatta kumnyima stakabadhi alizotaka ilikuimarisha kesi dhidi ya kiongozi huyo wa Kenya.

Bw Kenyatta kwa upande wake naye alikuwa amewasilisha ombi mahakamani ya kutaka kesi dhidi yake itupiliwe mbali baada ya bi Bensouda kukiri kuwa hakuwa na ushahidi wa kutosha dhidi yake.