MGONJWA BANDIA AKAMATWA NA POLISI


Mwanamume mmoja ameshtakiwa kwa kosa la kutumia udanganyifu na kujidai kuwa mgonjwa mahututi kwa miaka miwili nchini Uingereza ili kukwepa mkono wa sheria.

Mwanamume huyo kwa jina Alan Knight, mwenye umri wa miaka 47, kutoka mtaa wa Swansea,aliamua kujidai kuwa mgonjwa baada ya kushtakiwa na polisi kwa kosa la kumuibia mzee mmoja jirani yake pauni elfu arobaini.

Pindi alipogundua kuwa alikuwa anasakwa na polisi, Knight alikwenda hospitalini kwa kutumia kiti cha magurudumu akiwa anatumia gesi ya Oxygen na kudangaya kuwa hawezi kutembea kutokana na kupooza kutoka shingoni hadi miguuni.

Hii ilikuwa njama yake ili asiweze kukamatwa kwa kosa hilo.

Knight na mkewe madukani
Kila wakati polisi walipotaka kumfikisha mahakamani , Knight alipelekwa na mkewe hositalini akidai kuwa amezidiwa.

Hata hivyo siku zake za mwizi kushikwa zilifika pale wauguzi walipompata katika chumba chake hospitalini akiwa anakula , kupanguza mdomo wake na hata kuandika.

Kwa miaka miwili, Knight alikwepa mkono wa sheria kwa kudai kuwa alikuwa hawezi kuamka wala kutembea na pia alikuwa tayari na uraibu wa kutumia gesi ya oxygen kama mtu ambaye hawezi kupumua bila usaidizi wa gesi hiyo.

Yote hayo yalikuwa uongo na ambayo yangewezekana tu kwa sinema.
Hapa Knight alinaswa kwa kamera ya CCTV na polisi akiwa madukani
Alan Knight, alinaswa na polisi kwa camera ya CCTV akisukuma gari la kubebea bidhaa ndani ya duka la Tesco wakati akijidai kuwa mgonjwa mahututi.

Afisaa mmoja wa polisi Paul Harry,kutoka South Wales alisema: ‘Katika kazi yangu hii, sijawahi kuona kisa kama hicho ambacho kilipangwa na kutekelezwa kwa umaakini huo.''
Mkewe Knight ndiye alikuwa msaidizi wake katika sakata hii akimhudumia wakati wote
Mkewe Knight mwenye watoto watatu , pia alikuwemo kwenye sakata hiyo kwani siku zote alionekana akimhudumia mumewe aliyejidai kuwa hali mahututi.

Mbunge wa eneo la Swansea West aliambia BBC kuwa: "Nilikutana na Bi Hellen na akaniarufu ambavyo mumewe alikuwa na hali mbaya ya kiafya na kwamba walitendewa vibaya na polisi.''

Knight anakabiliwa na mashitaka 19 ikiwemo wizi na ikiwa atapatikana na hatia huenda akafungwa jela.