CCM: NDOA YA UKAWA FEKI

Makamu Mwenyekiti Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Philip Mangula amesema, hatua ya vyama vya upinzani vya kundi linalojiita Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kuungana rasmi, Dar es Salaam si jambo jipya.


Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Mangula alisema hii si mara ya kwanza kwa vyama hivyo kuungana na kwamba hatua hiyo haitaweza kubadilisha uwezo wa chama tawala cha CCM.

Alisema mwaka 2000 waliungana katika viwanja vya Kidongo Chekundu jijini Dar es Salaam na kurusha njiwa na mara ya pili walikutana hoteli ya Travertine, Magomeni katika kikao chao cha ndani na kupeperusha bendera za kuungana.

“Katika kikao hicho nilialikwa…kila mmoja alikuwa na bendera na wakakubaliana kuungana,” alisema Mangula akisisitiza kuwa kama muungano huo utakuwa na nguvu ni mzuri, kwani hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema Tanzania inahitaji upinzani imara.

Alisema muungano huo wa Ukawa hauwezi kupunguza idadi ya mashina, matawi na hata kata zinazoongozwa na CCM, kwani hata katika matokeo ya uchaguzi kuanzia mwaka 1995, matokeo yake yako wazi kuwa hawakuweza.

Mangula alitoa mfano uchaguzi wa mwaka 1995 katika nafasi ya Urais, kwamba alishinda mgombea wa CCM kwa asilimia 61.8, mwaka 2000 mgombea wa CCM alishinda kwa asilimia 71 na mwaka 2005 kwa asilimia 80, jambo linaloonesha wazi kuwa muungano huo wa wapinzani, hauwezi kubadilisha chochote.

Aidha, alisema hatua hiyo ni faida kwa CCM, ambayo itakutana na wagombea wachache, wakiwania nafasi mbalimbali za uongozi katika chaguzi zijazo, jambo litakalowapa urahisi zaidi wa kuchuana.

Mangula alisema CCM inatoa ofa kwa Ukawa, kuwa endapo watashindwa kumpata mgombea wa ngazi ya Urais mwenye vigezo vinavyotakiwa, wao wako tayari kuwaazima ili kuweza kujaza nafasi hiyo.

Vyama vilivyoungana juzi ni Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.


Chanzo: Habari Leo