RAIS KIKWETE KUKABIDHIWA KATIBA ILIYOPENDEKEZWA

HISTORIA inaandikwa nchini kutokana na kukamilika kwa sehemu kubwa ya mchakato wa kutengeneza Katiba mpya kutokanana leo Katiba Inayopendekezwa kukabidhiwa kwa Rais kabla ya ngwe ya mwisho ya kura ya maoni.

Tukio hilo la kihistoria linafanyika mjini Dodoma likitarajiwa kuhudhuriwa na watu wa kada tofauti wakiwamo mabalozi wa nchi karibu zote ambao wamealikwa.

Kwenye sherehe hizo ambazo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Ally Mohamed Shein watakabidhiwa Katiba hiyo huku polisi mkoani Dodoma ikiwahakikishia umma usalama wa kutosha.Akizungumza na gazeti hili, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mkumbwa Ally alisema "Tumealikamabalozi wa nchi karibu zote…sijajua waliothibitisha kufika ingawa hakuna aliyetoa udhuru.

"Licha ya mabalozi wanaotarajiwa kutoka nchi mbalimbali, kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Rehema Nchimbi, sherehe hizo zitahudhuriwa pia na viongozi kutoka nje ya nchi. Pia kutakuwa naviongozi wakuu wastaafu, viongozi wa dini na wananchi kwa ujumla.

Usalama Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema ulinzi umeimarishwa katika maeneo yote ya mji.

Alisema zinafanyika doria kwa miguu, mbwa, farasi, magari na pikipiki kuhakikisha sherehe hizo zinafanyika kwa utulivu mkubwa.

Pia wamiliki wa nyumba za wageni wametakiwa kuimarisha ulinzi. Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Kamanda alisema ufuatiliaji wa taarifa mbalimbali nakuzifanyia kazi umeimarishwa zaidi.
Kamanda Misime alisema vyombo vyote vya dola vimeimarisha zaidi ushirikiano hasa kubadilishana taarifa mbalimbali na kufuatilia tukio hilo muhimu kwa kutumia mbinu zote walizo nazo.

"Niwahakikishie wananchi wa Mkoawa Dodoma na wageni wote kuwa ulinzi na usalama umeimarishwa; Tunachowaomba ni ushirikiano wao pale watakapomtilia mashaka mtu yeyote au jambo lolote wajulishe Polisi haraka nasi tutalifanyia kazi," alisema Misime.

Pia wenye nyumba za kulala wageni, pamoja na kuimarisha ulinzi kwenye maeneo yao, wameelekezwa wakitilia mashaka mgeni yeyote watoe taarifa Polisi.

Alihadharisha kwa kusema anayepanga kukiuka sheria kwa lengo la kuvunja amani na utulivu, atashurutishwa kwa nguvu kwa mujibu wa sheria za nchi na kwa mamlaka iliyopewa jeshi lake.

Safari ya Katiba mpya Hatua mbalimbali zimepitiwa kabla ya kupatikana Katiba Inayopendekezwa Oktoba 2, 2014 iliyopitishwa kwa kura zinazostahili. Mchakato wa kupata Katiba mpya ulianza na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba iliyopitishwa bungeni Novemba, 2011 na kufanyiwa mabadiliko Februari, 2012.

Rais Jakaya Kikwete aliunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa mujibu wa Kifungu 6(1) cha sheria hiyo.
Wajumbe 34 wa Tume waliteuliwa na kuapishwa na Rais Kikwete, Aprili, 2012 na ikapewa miezi 18 kukamilisha kazi yake kuanzia siku ilipoanza kazi rasmi ambayo ilikuwa Mei 2, 2012. Uzinduzi wa Rasimu ya Katiba Mpya ulifanyika Juni 3, mwaka jana katika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.

Bunge Maalumu la Katiba lilianza Februari mwaka huu. Lilikwenda hadi Aprili kabla ya kuahirishwa kupisha Bunge la Bajeti na kisha kuanza awamu nyingine Agosti 5 mwaka huu.

Hata hivyo, sehemu ya wajumbe wa bunge hilo wanaojiita Umoja wa Wabunge wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), walisusa ingawa mchakato ulioendelea hadi Oktoba 2, mwaka huu ilipopatikana Katiba Inayopendekezwa.
Kususa kwa kundi hilo, hakukuathiri mchakato huo kuendelea lakini umechelewesha hatua inayofuata kwa kuwa baada ya kupatikana Katiba Inayopendekezwa, hatua nyingine ingekuwa Kura ya Maoni.

Lakini kulingana na makubaliano yaliyofanyika hivi karibuni kati ya Rais Kikwete na viongozi wa vyama vinavyounda Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), mchakato wa kura ya maoni utafanyika baada ya uchaguzi mkuu mwakani; kwa maana utategemea utashi wa rais ajaye.

Walikubaliana kwamba kwa mujibuwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, baada ya bunge hilo kumaliza kutunga Katiba, ingefuata hatua ya kura ya maoni kuthibitisha Katiba.

Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo alisema walikubaliana kwamba kwakutambua kuwa hatua ya kura ya maoni italazimisha uchaguzi mkuu 2015 kuahirishwa, basi hatua hii iahirishwe na mchakato wa Katiba uendelee baada ya uchaguzi mkuu.

Wakati huohuo, msemaji wa Ukawa ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi, James Mbatia alisema:
"Hatutahudhuria, kwa sababu hatuna mwaliko, sisi ni taasisi, kama mabalozi wamealikwa na watu wengine kwenye sherehe hiyo, na sisi tungealikwa kwa barua".

Hata hivyo, alipoulizwa ikiwa wangepata mwaliko kama wangehudhuria, Mbatia alisema ingetegemea na maudhui ya baruaya mwaliko na kwamba hawezi kuzungumzia zaidi kwa kuwa hana huo mwaliko.

Kwa upande wao, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Dk Willbrod Slaa kimesema kinachambua Katiba Inayopendekezwa na nyaraka nyingine kwa ajili ya kuzunguka nchi nzima kuipinga kwa wananchi.

Dk Slaa alisisitiza chama chake pamoja na vyama vingine vinavyounda Ukawa, kutohudhuria sherehe hizo za kukabidhiwa kwa Katiba Inayopendekezwa.

"Hatuko tayari sisi Chadema wala Ukawa kuhudhuria sherehe hizo Dodoma," alisema.



Chanzo: Habari Leo