WATU WATATU WAKAMATWA USAFIRISHAJI HARAMU WA BINADAMU

Watanzania watatu wanashikiliwa na jeshi la polisi Mkoani Tanga wakituhumiwa kuendesha biashara ya kuwasafirisha kwa kutumia gari aina ya hiace wahamiaji haramu 10 kutoka nchini Ethiopia.

Kamanda wa Polisi Mkoani Tanga ,Leonard Paulo amesema leo kuwa watanzania hao pamoja nawahabeshi wamekamatwa jana saa 2.30 usiku katika eneo la Misajini barabara kuu ya Hedaru- Mombo.

Amesema kuwa wahamiaji hao walimatwa wakati askari wakiwa doria waliokuwa wakisafirishwa kwenye gari aina Toyota Hiace iliyokuwa ikiendeshwa na Ally Juma (24) mkazi wa Dar es Salaam wakiingia mkoani hapa.

Amewataja watanzania wengine wawili ambao wamekamatwa wakituhumiwa kuwakisafirisha wahamiaji haramu hao kuwa ni Joseph John (42) mkazi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Iddi Juma(38) mkazi wa mkoani Iringa.

Ametaja majina ya Wahabeshi waliokuwa wakisafirishwa kuwa ni
Tarfa Wolder (21),Aramei Yonas (21),Gazae Edson(20),Yohanes Abakar (27),Anemo Tamire (16),Indira Yaiso(18),Wasifimu Paresa (15),Dedacho Gadam (20),Tamelata Abala (17) na Mlatu Shugute (32).

RAIS NKURUNZINZA AMTUMIA RAIS DK. MAGUFULI UJUMBE

Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza amemuomba Rais John Magufuli kuwasihi wananchi wake waliokimbia nchini humo, kurejea akimhakikishia kuwa hali ni shwari.

Baadhi ya Warundi waliikimbia nchi hiyo wakihofia maisha yao kutokana na vurugu za kisiasa zilizotokea wakati wa uchaguzi mkuu baada ya kupinga kiongozi huyo kugombea tena.

Katika ujumbe uliowasilishwa Ikulu, jana na Mnadhimu wa Jeshi la Burundi, Meja Jenerali Evariste Ndayishimiye ambaye ni mjumbe maalumu wa Rais Nkurunziza, kiongozi huyo alimuomba Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kuwasihi wananchi wa Burundi waliokimbia nchi yao warejee nyumbani.

Meja Jenerali Ndayishimiye alimueleza Rais Magufuli kwamba ametumwa kuleta barua hiyo pamoja na shukrani za dhati kwa Tanzania ambayo ni rafiki, jirani na ndugu wa kweli wa Burundi kwa ushirikiano mzuri inaoupata.

Dk Magufuli alimshukuru Rais Nkurunziza kwa ujumbe huo na kumhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kuwa rafiki na ndugu wa dhati wa Burundi.

Kuhusu hali ya Burundi, Rais Magufuli alisema anaamini kuwa wasuluhishi mgogoro wa nchi hiyo; Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa watafanikiwa kuusuluhisha.


Chanzo:Mwananchi