NDUGU WADAIWA KUNYONGWA

Watu wasiojulikana wamewanyonga hadi kufa ndugu wawili wakazi wa maeneo ya Mtaa wa Madafu, Tandika jijini hapa.

Ndugu hao, Mwakamu Mariamu Buruhani (39) na Nuru Tumwanga (42) walinyongwa usiku wa kuamkia jana.
Kwa mujibuwa habari ambazo Mwananchi imezipata, Mwakamu ni mmiliki wa saluni iliyopo mtaa huo na inayoitwa Hair dressing.
Mmoja wa wafanyakazi wa saluni hiyo alidokeza kuwa, baada ya kuona muda wa kufungua umepita, alimtuma kijana kwenda kumwangalia Mwakamu na kumhimiza aje wafungue saluni hiyo.
Mfanyakazi huyo alisema kijana huyo alipofika alikuta mlango uko wazi na Nuru alikuwa kitandani na mwenzake sakafuni sebuleni na ndipo alipokwenda kumwita mwenyekiti wa Serikali za Mitaa, Mtaa wa Mji Mpya, Wadadi Mtangwa na kisha kutoa taarifa polisi.
Polisi walifika na kuichukua miili hiyo na kuipeleka Hospitali ya Temeke na uchunguzi wa awali ulibaini kuwa wamenyongwa kwa kuwa walikuwa na michubuko shingoni. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Kihenya wa Kihenya, alikiri kutokea tukio hilo.