NAFUU KWA WALIMU AJIRA ZAIDI KUTANGAZWA

SERIKALI imetangaza kutoa ajira mpya 26,000 za walimu kuanzia Januari mwakani, ikiwa ni mpango endelevu wa kupunguza uhaba wa walimu katika shule za msingi na sekondari nchini.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), anayeshughulikia Elimu, Kassim Majaliwa, alisema hayo juzi mjini hapa wakati akifunga kikao cha kazicha siku tatu cha maofisa elimu wamikoa na halmashauri za wilaya nchini, wanaosimamia elimu ya msingi.

"Serikali inatambua uhaba wa walimu na kila mwaka inatoa ajira mpya za walimu. Januari 2014 Serikali itatoa ajira 26,000 za walimu wapya na maelekezo mengine yatafuata," alisema Majaliwa.

Aliwataka maofisa elimu hao kuzingatia uwiano wa walimu wakati wa kuwapangia vituo vya kazi, badala ya kuendelea kuwalundika maeneo ya shule za mijini pekee.

Pia aliagiza walimu hao watayarishiwe mazingira mazuri hasa katika maeneo ya pembezoni kwa kuwapatia motisha, ili kuwajengea moyo wa kufanya kazi kwa bidii na maarifa zaidi katika vituo vyao vya kazi kwa lengo la kuwafanya wasikimbie vituo.

Licha ya kutangaza ajira hizo mpya, Majaliwa pia alisema Serikali imetenga Sh bilioni 18 za kutengeneza madawati yatakayo sambazwa shuleni na zabuni yake inatarajiwa kutangazwa mapema iwezekanavyo.

Alisema mpango huo unatarajia kuanza mapema mwakani baada yakumpata mzabuni, "najua kutokanana kiwango kidogo cha fedha, hatutaweza kutosheleza, lakini huuni mwanzo."

Aliwataka maofisa hao kujenga tabia ya ufuatiliaji shuleni, ili kusimamia utunzaji wa vifaa na wakikuta uzembe ni wajibu wao kuchukua hatua ya kumaliza matatizo yaliyo chini na uwezo wao.