Inadaiwa siku chache kabla ya maziko ya Mandela, mjukuu wake mkubwa, Mandla alifukuzwa katika nyumba ya babu yake katika kijiji cha Qunu.
Mbali na kufukuzwa, inadaiwa vitasa vya nyumba hiyo vilibadilishwa na huduma za maji na umeme zilizokuwa zikitumika katika nyumba ya Mandla kijijini hapo, zilisitishwa.
Hata usafiri kwa ajili ya kwenda mazikoni haukutolewa kwa ndugu waliozaliwa pamoja na Mandla na wanasiasa na viongozi wa dini waliokuwa wakishirikiana na mjukuu huyo, walitengwa na wengine kukosa mwaliko wa kuhudhuria maziko ya Jumapili.
Inadaiwa kwamba mtoto mkubwa wa kike wa Mandela, Makaziwe, alimtaka Mandla, ambaye ni Chifu wa Mvezo, kijiji alichozaliwa Mandela, kutoa mifugo yake iliyokuwa katika eneo la nyumba hiyo.
Gazeti la The Times, limebainisha kwamba mjane wa Mandela, Graca Machel na mwanasheria wa siku nyingi wa kiongozi huyo, George Bizos, walijaribu kuwataka wanafamilia hao kudhibiti hali hiyo isijioneshe lakini bila mafanikio.
Kiini Ugomvi huo ulitokana na mgogoro ulioibuka wakati Mandela akiwa mahututi katika Hospitali ya Med Clinic, kuhusu wapi alipaswa kuzikwa kati ya kijiji alichozaliwa cha Mvezo au alichokulia cha Qunu.
Wosia wa Mandela uliofunguliwa akiwa katika hospitali hiyo ya Pretoria, ulieleza wazi kuwa alipenda azikwe karibu na wanawe walikozikwa na kwa wakati huo, makaburi yao yalikuwa Mvezo.
Wanawe hao, Makgato aliyefariki dunia mwaka 2005; Makaziwe, ambaye ni mwanawe wa kike wa kwanza aliyefariki dunia akiwa mchanga mwaka 1948; na Madiba Thembekilea, aliyekufa kwa ajali yagari mwaka 1969; walizikwa Qunu.
Hata hivyo, Mandla, ambaye ni mtoto wa Makgato na kiongozi mkuu wa ukoo wa Madiba, anaotoka Mandela na Mbunge wa ANC, alifukua miili hiyo mwaka 2011 na kuizika upya Mvezo, alikozaliwa babu yake.
Mahakamani Uamuzi huo wa Mandla ambao haukushirikisha familia, ulisababisha watoto wa Mandela, wakiwakilishwa na Mwanasheria, Sandla Zigadla, kwenda mahakamani kutaka mabaki ya ndugu zao, yarudishwe Qunu.Jaji Lusindiso Pakade, alitoa amri kumtaka Mandla aache kuingilia mchakato wa kuhamisha mabaki yamiili hiyo kutoka Mvezo kwenda Qunu.
Mandla alifanya jaribio la kuzuia mchakato huo, lakini Jaji Pakade, alizuia jaribio hilo na badala yake akakazia hukumu kutaka miili hiyo ifukuliwe haraka.
Nguvu yatumika Baada ya hukumu hiyo, huku vyombo vya habari vya Afrika Kusini na kimataifa vikishuhudia, maofisa wa Serikali walivunja lango la makazi ya Mandla kwa vifaa maalumu, ili kutoa nafasi kwa gari la kubeba maiti kuingia ndani yalikokuwa makaburi hayo.
Miili ilifukuliwa na uchunguzi wa kisayansi kufanyika kwa takribani saa mbili na kuthibitisha kwamba ni mabaki ya watoto hao, kabla ya kuzikwa upya Qunu.Juzi, Mandla alisema:
"Kama ilivyo kwa karibu kila mmoja wetu katika familia, kabla ya kifo cha babu, nilidhamiria kutoomboleza, nilijiandaa kusherehekea mazuri yote aliyoniachia na aliyoacha kwa ajili ya ulimwengu.
"Hata hivyo, nilikosea, kwa kuwa maumivu ya kumpoteza tata bila kutarajia, yaliniingia kama vile niliyekatwa nakitu chenye ncha kali."
Mjukuu huyo, alisema alijikuta akiugua upweke siku chache baada ya kifo cha Madiba, pamoja na kuwa karibu na familia.
"Hata hivyo ujumbe wa kututakia faraja ulivyokuwa ukitufikia, nilianza kupona," alisema Mandla. Pia alishukuru Serikali kwa kuandaa masuala yaliyokuwa yakifanyika katika siku hizo 10 za maombolezo na kuongeza kuwa kila kitu kilifanyika vizuri.