Bibi kizee mmoja mwenye umri wa mika 65 ameuawa kikatili kwa kukatwa vibaya katika maeneo mbalimbali ya mwili wake na kusababisha kifo chake katika eneo la Kigogo Mburahati national housing jijini Dar es Salaam.
Kutokana na tukio hilo la kikatili aliofanyiwa bibi huyo kizee aliyefahamika kwa jina na Bi Asia Mohamed maarufu kwa jina la bibi Chadego, ITV ilifika nyumbani kwa bibi huyo mwenye umri wa miaka 65 na kuzungumza na mjumbe wa eneo hilo bi Hidaya Salum na kusema bibi huyo ameuawa kikatili akiwa nyumbani kwake huku mtoto wa marehemu naye akieleza kusikitishwa na kifo cha mama yake.
Baadhi ya wasamaria wema ambao hawakutaka kutaja majina yao kwa usalama wao.
Wamesema bibi huyo alikuwa akihusishwa na mambo ya ushirikina na baadhi ya familia yake baada ya vifo vya wajukuu wake watatu ambao walifariki kwa nyakati tofauti kipindi cha nyuma ambao licha ya kudaiwa wajukuu hao kufariki kwa mambo ya kishirikina lakini ukweli ni kwamba bibi huyo hakuwa mchawi wala hakuhusika na vifo hivyo huku ikidaiwa kwamba bibi huyo hakuuawa na mjukuu wake kama inavyodaiwa ila kuna mchezo uliochezwa na watu fulani ili kumuua na kisha kugeuza kuwa ni mjukuu wake mwenye tatizo la akili.
Kamishna msaidizi wa polisi kutoka mkoa wa kipolisi kinondoni ACP Camilius Wambura, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba licha ya mjukuu wa bibi huyo kushikiliwa na jeshi la polisi kwa madai ya upotevu wa godoro lakini upepelezi wa uhakika bado unaendelea kuhusu tukio hilo hivyo wananchi wameombwa kutoa ushirikiano ambapo pia mganga mkuu wa hospitali ya mwananyamala dakta Sophinias ngonyani amekiri mwili wa marehemu kuhifadhiwa katika hospitali hiyo.
Chanzo:ITV