WATU SITA WAMEKUFA BAADA YA KUFUKIWA NA KIFUSI

WATU sita wakiwemo wanafunzi wawili wamekufa papo hapo na wengine watatu kujeruhiwa, baada ya kufukiwa na kifusi wakati wakichimba mchanga katika eneo la Pumwani wilayani Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro. Tayari serikali imeyafunga machimbo yote mkoani humo yakiwamo yaliyosababisha vifo hivyo, ili kuepusha athari zaidi kwa wachimbaji wengine, ikizingatiwa kuna mvua za vuli zinazoendelea maeneo mbalimbali nchini.

Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Robert Boaz amethibitisha kuwapo kwa tukio hilo la juzi majira ya saa 10.30 jioni wakati wachimbaji hao wakichimba mchanga kwa ajili ya biashara.

Waliofariki wametajwa kuwa ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Ebenezer –Sango, David Macha (18)na Marwa Mwita (14) aliyechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Uparo.

Wanafunzi hao walikuwa wakifanya vibarua vya kuchimba mchanga kwa ajili ya kutafuta fedha za kujikimu pamoja na kusaidia maendeleo ya kitaaluma katika shule walizokuwa wakisoma.

Wengie waliofariki ni Ephraim Assei (27), mkazi wa Kawawa, Ludovick Venance (16), Omari Masoud (33) na Augustine Lyimo (26), wote wakazi wa Pumwani ambao miili yao imehifadhiwa hospitali ya mkoa ya Mawenzi.

Kamanda aliwataja waliojeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi ni dereva wa lori aina ya Mitsubishi Fuso lenye namba za usajili T 167 AQG, Antipus Babu (56), ambaye alipata majeraha kichwani.

Wengine ni utingo wa lori hilo, Simon Mosha (21), aliyepata majeraha madogo na kutibiwa eneo la tukio huku mtu mwingine aliyejulikana kwa jina moja la Charles (30), mkazi wa Sango akiwa amejeruhiwa vibaya.

Alisema Charles amelazwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) katika Hospitali ya KCMC.

Kamanda alitoa tahadhari kwa wakazi wa maeneo yote yanayochimbwa mchanga na moramu kuepuka kufanya kazi hiyo kienyeji, hususani kipindi hiki cha mvua za vuli.Hata hivyo baada ya kutokea kwa tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Dk Ibrahim Msengi ni miongoni mwa watu waliosaidia zoezi la uopoaji wa miili ya waliokufa.

Gama alitangaza kufungwa kwa machimbo hayo na kutaka wataalamu wa ofisi ya madini Kanda ya Kaskazini waliopo mkoaniArusha kupima eneo hilo iwapo linastahili kuendelea na uchimbaji wa mchanga au la.

Mkuu wa mkoa ambaye aliambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo, alisema pamoja na eneo hilo, lakini pia machimbo mengine yote mkoani humo ikiwamo ya moramu nayo yanasimamishwa hadi yapimwe.