MAUWAJI MAKUBWA YARIPOTIWA SUDAN KUSINI

Taarifa mpya zimeibuka zikieleza kuwepo kwa mauaji ya kikabila yaliyofanyika katika kipindi cha zaidi ya wiki moja ya ghasia nchini Sudan Kusini.

Mwandishi wa habari mmoja kutoka mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, amewakariri watu walioshuhudia mauaji hayo wakisema zaidi ya watu 200, wengi wao wakitoka kabila la Nuer , wameuawa kwa kupigwa risasi na majeshi ya usalama.

Mtu mwingine kutoka Juba amesema watu wenye silaha kutoka kabila la Dinka walikuwa wakiwashambulia kwa risasi watu kutoka maeneo ya Nuer.

Ghasia hizo zimekuja huku kukiwa na hali ya kugombea madaraka kati ya Rais Salva Kiir, kutoka kabila la Dinka, na aliyekuwa naibu wake Riek Machar kutoka kabila la Nuer.

Serikali ya Sudan Kusini imekanusha kuhusika na ghasia za kikabila.

Taarifa hizo zimekuja wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akitoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuongeza askari 5,500wa Umoja wa Mataifa katika kikosi cha askari 7,000 wa Umoja wa Mataifa waliopo Sudan Kusini.

Waasi wanaomuunga mkono makamu wa rais aliyefukuzwa Riek Machar walitwaa miji mikubwa wiki iliyopita.

Maelfu ya watu wamekimbia mapigano.