MAELFU WAJITOKEZA KUMUAGA MANDELA

Rais wa Marekani Barack Obama na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon watakuwa miongoni mwa viongozi wa dunia watakaohutubia muhadhara huo.

Viongozi hao pia watahutubia wananchi sawa na wajukuu wanne wa Mandela.

Maelfu ya watu wamehudhuria misa hiyo katika uwanja wa FNB.

Afrika Kusini imeandaa shughuli mbali mbali za kumuenzi Mandela kabla ya siku ya kuzikwa kwake nchini Afrika Kusini siku ya Jumapili.

Misa ya leo ni moja ya mikusanyiko mikubwa ya viongozi wa kimataifa iliyoshuhudiwa nchini humo katika miaka ya hivi karibuni.

Viongozi wanaohudhuria misa ya wafu ya Mandela
Rais wa Marekani Barack Obama
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon
Rais wa Cuba Raul Castro
Rais wa Ufaransa Francois Hollande
Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron
Rais wa Brazil Dilma Rousseff
Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe
Watu wengi wamekaidi hali mbaya ya hewa ambapo mvua kubwa imenyesha huku wakikusanyika uwanjani humo wakisubiri kwa muda mrefu kabla ya misa hiyo kuanza muda mfupi uliopita.

Waliohudhuria misa hiyo wamesemekana kuwa wenye furaha wakiimba nyimbo na kutaja jina la Mandela kwa shangwe unaweza kudhani ni mkutano wa kisiasa.

Misa hiyo itafanyika katika uwanja ambako Nelson Mandela alionekana kwa mara ya mwisho hadharani.

Misa hiyo itaonyeshwa kwenye skrini kubwa nje ya uwanja ili kuzuia msongamano wa watu.

Mandela alifariki akiwa na umri wa miaka 95 na kwa wengi yeye ni shujaa na mkombozi wa Afrika Kusini.