ALIYEKUWA MAKAMU WA RAIS SUDAN KUSINI AKANA JARIBIO LA MAPINDUZI

Aliyekuwa makamu wa Rais wa Sudan Kusini Riek Machar aliyekimbilia mafichoni amekataamadai kuwa amehusika katika jaribio la mapinduzi.

Ameiambia BBC kuwa wa kulaumiwa kwa machafuko yaliyotokea katika mji mkuu wa Juba ni rais Salva Kiir ambaye anadai kuhusika kwake.

Machar ambae alifarakana na Rais Salva Kiir mnamo mwezi wa Julai alimshtumu kwa "kuchochea mapigano ya kikabilai" ili kuficha udhaifu wake.. Rais Kiir amesema kikundi cha wanajeshi wanaomuunga mkono Bwana Machar kilijaribu kutwaa madaraka kwa nguvu usiku wa Jumaapili lakini walishindwa.

Alisema mapigano hayo yalianza pale watu waliovalia mavazi ya kijeshi walipofyatua risasi katika mkuano wa chama kinachotawala cha (SPLM). Lakini Bw Machar aliiambia BBC: "Hakukuwepo jaribio lolote la mapinduzi."

Rais wa baraza la usalama la umoja wa mataifa Gerard Arud amesema kuwa mzozo unaoendelea nchini Sudan Kusini ambao umechukua mrengo wa kikabila unaweza kugeuka na kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Bwana Arud ameiambia BBC kwamba umoja wa mataifa umepata habari kwamba mamia ya watu tayari wamepoteza maisha yao tangia jaribio la mapinduzi lifanyike siku ya jumapili, ijapokuwa amesisitiza kuwa sio raia wanaolengwa.

Ameiambia BBC kwamba takriban raia elfu 20 wamepewa hifadhi katika makao ya umoja wa mataifa katika mji wa Juba na kwamba wanakumbwa na uhaba wa chakula na madawa.