SERIKALI YA DRC NA M23 WASAINI MKATABA WA AMANI

Serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo hatimaye imesaini mkataba wa amani na waasi wa kundi la M23 waliokuwa wakifanya mashambulio ya mara kwa mara mashariki mwa nchi hiyo.

Waasi wa M23 walijilsalimisha mwezi uliopita baada ya kushindwa katika oparesheni iliyoendeshwa na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasiaya Congo ikisaidiwa na majeshi ya Umoja wa Mataifa.

Alhamisi, maraisYuweri Museveni, ambaye ndiye mwenyekiti wa kongamano la kimataifa juu ya usalama katika maziwa makuu, na Joyce Banda, raiswa Malawi, ambaye ndiye mwenyekiti wa jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika SADC, walisaini kama wadhamini wamkataba huo.

Marais hao walisaini mkataba huo wakiwa jijini Nairobi walikohudhuria sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa Kenya.

Makubaliano

>Kundi la M23 limeweka rasmi katika mkataba huo kuwa watasitisha maasi yote na kulivunja kundi lao kama vugu vugu la waasi na badala yake kusukuma ajenda zake kupitia njia za kisiasa.

>Serikali ya Congo nayo imeweka masharti ya kutolewa msamaha kwa waasi hao na mpango wa kupokonywa silaha wote wanaojisalimisha kutoka kwa kundi hilo.

>Serikali hiyo pia imekataa kuwa jumuisha kijumla waasi wote waliojiondoa kutoka M23, katika jeshi lake.

Safari ndefu

Juhudi za awali kutafuta amani kati ya serikali ya DRC na waasi hao wa M23 zilishindikana.
Mwaka mzima baadaye, licha ya kuandikwa mkataba huo, pande mbili zilikataa kusaini kutokana na kushindwa kukubaliana jina litakalopewa. Upande wa serikali ya DRC ulisisitiza kuwa hakuna mkataba wa amani na waasi, hasa baada ya kuwa wamewashinda vitani.

Tangu kupigwa na kufukuzwa kwa waasi hao kutoka mkoa wa Kivu ya kaskazini, waasi hao wa M23 wamekuwa wakijisalimisha kwa serikali ya Uganda na kuomba hifadhi. Serikali ya DRC imetaka warudishwe nchini humo ili wakabiliwe na mashtaka ya mauaji, ubakaji na uhalifu mwinigne wa kivita. Hata hivyo Uganda imekataa kuwakabidhi ikisema kuwa ni wakimbizi wanaosubiri uamuzi kutoka shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi, UNHCR.

Hadi sasa amani imeanza kurejea katika maeneo yaliyokombolewa kutoka mikono ya waasi wa M23.

Hata hivyo mwandishi wa BBC katika eneo hilo Lubunga Bya Ombe, anasema kuwa bado serikali hiyo ya DRC ina kibarua kigumu kukabili makundi mengine madogo ya waasi yaliyo kita kambi katika eneo hilo.

Wiki hii serikali ya DRC ikishirikiana na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa imetangaza oparesheni mpya dhidi ya Kundi la waasi la FDLR.

Masuala tete

Lakini masuala mengine yamesalia bila kutatuliwa. Mfano, bado haijulikani serikali ya DRC itachukua hatua gani kwa baadhi ya viongozi wa Kundi hilo la M23, ambao hawapati msamaha kutokana na kuwa wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji, ubakaji na uhalifu wa kivita.Viongozi hao wameorodheshwa katika orodha ya jamii ya kimataifa ya wahalifu wa kivita.

Miongoni mwa viongozi wa kundi hilo ambao hawajapewa msamaha ni aliyekuwa kiongozi wao Askofu Runiga, Brg. Jenerali Bouduain Ngaruye na Kanali Sultan Makenga na wengineo Pia haijabainaka wazi hatma ya zaidiya waasi wa zamani 1500 wa M23 waliojisalimisha nchini Uganda iwapo watarudi Congo au la.