Chelsea ilimiliki mchezo huo kwamuda mrefu katika dakika zote 90, huku Chelsea ikipata goli kutokana na mchezaji wa Sunderland, Lee Cattermole kujifunga mwenyewe.
Chelsea walionekana kufuzu kucheza hatua ya nusu fainali hadi dakika za mwisho za mchezo, lakini ndoto hiyo ilizimwa na Fabio Borini aliyesawazisha goli dakika ya 88 na kulazimisha mchezo huo kuingia muda wa ziada.
Sunderland ilipigana na kufanikiwa kupata bao la ushindi katika dakika ya 118 likifungwa na Ki Sung-Yueng.
Muda wa ziada ulizidi kumkoroga kocha wa Chelsea Jose Mourinho, ambaye tayari amekuwa akilalamikia ratiba ya michezo kuibana timu yake, akionyesha kuwa Arsenal ina siku zaidi za kupumzika kulinganisha na wao katika kujiandaa kwa mchezo watakaopambana na Arsenal katika mechi za Ligi Kuu ya England, Jumatatu.
Matokeo mengine ni Manchester City kuichapa Leicester mabao 3-1. Magoli ya ManCity yamefungwa na Kolarov dakika ya8 na Dzeko akifunga katika dakikaza 41 na 53. Bao la kufutia machozi kwa Leicester limetumbukizwa kimiani na Dyerkatika dakika ya 77.