Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Tarek Mitri, ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa timu ya shirika la kimataifa la nguvu za nyuklia,IAEA, litawasili nchini humo baadaye mwezi huu.
Amesema mapipa 6,400 ya malighafi ya Uranium, maarufu kama keki ya manjano, yalihifadhiwa katika kambi ya zamani ya kijeshi kusini mwa Libya, yakilindwa na kikosi cha jeshi.
Mali ghafi hiyo inatumika katika uzalishaji wa nishati na silaha za nyuklia.
Bwana Mitri, mwakilishi maalum waKatibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, amesema timu ya wakaguzi kutoka IAEA watatembelea Libya mwezi huu kuthibitisha kiasi cha nyuklia kilichohifadhiwa na hali ya sehemu ilipohifadhiwa katika kambi ya zamani ya kijeshi karibu na mji wa Sabha, kusini mwa Libya. "Malighafi hiyo ya nyuklia inadhibitiwa na kikosi cha jeshi" amesema.
Wataalam kutoka IAEA walitembelea eneo la Sabha mwaka2011, muda mfupi baada ya kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Libya.
Bwana Mitri alikuwa akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati huu ambapo wasiwasi umekuwa ukiongezeka juu ya serikali ya Libya kushindwa kudhibiti vikundi vya wapiganaji ambavyo vimepata ushswishi na udhibiti katika miji muhimu tangu kuondolewa madarakani kwa Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011.