TANZANIA YAPAA VIWANGO VYA FIFA

TANZANIA imezidi kupaa kwenye viwango vya ubora wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) baada ya kupanda kwa nafasi nne na sasa ni ya 120 kutoka nafasi ya 124 mweziuliopita.

Viwango hivyo vimetoka ikiwa ni takribani wiki moja kupita tangu Tanzania itoke kwenye michuano ya Kombe la Chalenji inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) ambapo Bara ilishika nafasi ya nne na Zanzibar kuishia hatua ya makundi.

Kwa mujibu wa viwango hivyo vya FIFA, Uganda bado inaongoza katika ubora wa viwango kwa nchi wanachama wa Cecafa ikiwa nafasi ile ile ya 86 kama mwezi uliopita huku Ethiopia ikifuatia katika nafasiile ile ya 93.

Kenya inafuata ikiwa nafasi ya 109 na Sudan ni ya 119 huku Burundi ikishika nafasi ya 124, Rwanda ya 133, Eritrea ya 200, Sudan Kusini ya 201, Somalia ya 203 na Djiboutiya 204.

Ivory Coast inaendelea kuongoza kwa upande wa Afrika ikiwa nafasi ya 17 ikifuatiwa na Ghana katika nafasi ya 24 huku Algeria ikiwa ya 26. Nigeria ni ya 37, Misri ya 41, Mali ya 45, Cameroon iko katika nafasi ya 50, Burkina Faso ya 53, Libya ya 59 na Guinea ya 61.

Aidha katika viwango hivyo vya kufungia mwaka, nafasi kumi bora haijabadilika, Hispania ikiendelea kukaa kileleni ikifutiwa na Ujerumani na Argentina. Kwenye nafasi ya nne ikikaa Colombia, Ureno ni ya tano, kisha Uruguay.

Timu mbili za Asia zimepanda kwa kiwango kikubwa, Ufilipino (127 ikipanda kwa nafasi sita) na Guam (161, ikipanda nafasi nane 8).

Bingwa wa Ulaya na Dunia, Hispania inaongoza viwango hivyo kwa matoleo sita mfululizo, ikijiwekea mazingira mazuri ya kutwaa tuzo ya timu bora ya mwaka.

Timu iliyopanda kwa kiasi kikubwa katika viwango vya kumalizia mwaka, shukrani kwa ushindi wa mechi nane sare mbili, na kipigo kimoja ni Ukraine, ambayo imekusanya pointi 312 tangu Desemba 2012, ikipanda kwa nafasi 29 na sasa iko nafasi ya 18.

Pia ni mwaka wa mafanikio kwa Armenia (nafasi ya 35 ikikusanya pointi 259 tangu Desemba 2012) na Marekani USA (nafasi ya 14 ikikusanya pointi 237 tangu Desemba 2012).