Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Kamishna Dhahiri Kidavashari alisema mauaji hayo yalifanyika mkesha wa Sikukuu ya Krismasi , Desemba 24 katika kitongoji hicho cha Tulieni, Kata ya Itenka.
Kidavashari alimtaja mtuhumiwa wa mauaji hayo kuwa Mathias Mashini "Igoka' (46) mkazi wa kitongoji cha kijiji hicho cha Tulieni ambaye anadaiwa kuishi na mkewe huyo kwa miaka mingi bila kujaliwa watoto.
Akisimulia mkasa huo Kidavashari alidai kuwa kwa siku kadhaa wanandoa hao walikuwa wakishutumiana ambapo mke alikuwa akimshutumu mumewe kwa kushindwa kumpatia mahitaji muhimu ukiwemo unyumba kwa muda mrefu.
Inadaiwa kuwa baada ya kuoana mke alimkaribisha mumewe nyumbani kwake Tulieni na kufanya makazi.
Kwa mujibu wa Kidavashari, mke baada ya kuona mume haeleweki alimtaka mumewe huyo atoke nyumbani kwake (Rehema) kwa madai kuwa ameshindwa kumpatia mahitaji muhimu ukiwemo unyumba kwa muda mrefu kauli ambazo zilimkasirisha mume huyo ambaye inadaiwa hakuwa tayari kuachana na mkewe.
Inadaiwa mwanamke huyo alimfukuza mumewe huyo nyumbani hapo akisisitiza lazima aondoke ndipo mume huyo akishirikiana na mkazi wa kitongoji hicho aliyetambuliwa kwa jina la Ngussa Masengwa (39) walimshambulia mwanamke huyo kwa mapanga akiwa amelala nyumbani kwake hapo na kumjeruhi vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia umauti kisha waliufungia mwili wa marehemu ndani ya nyumba yake hiyo.
Kwa mujibu wa Kidavashari Siku ya Desemba 25 majirani baada ya kutowaona wanandoa hao huku nyumba yao ikiwa imefungwa mchana kutwa, waliamua kuwasiliana na Mathias kwa simu yake ya mkononi ambaye aliwaeleza kuwa wako Mpanda mjini wakila Sikukuu ya Krismasi.
Inadaiwa siku iliyofuata majirani wa wanandoa hao walianza kusikia harufu mbaya ikitokea ndani ya nyumba ya wanandoa hao ndipo walipolazimika kuvunja mlango wa nyumba hiyo na kushuhudia mwili wa marehemu ukiwa sakafuni.