Hata hivyo, washitakiwa hao kupitia kwa mawakili Richard Rweyongeza na Edward Chuwa, wamedai hati hiyo haijawasilishwa kwa usahihi kwa kuwa DPP amekosea kutumia sheria.
Washitakiwa hao wanakabiliwa na kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi katika Mahakama ya Hakimu MkaziKisutu, waliwasilisha ombi la dhamana katika Mahakama Kuu wakidai ni haki yao ya msingi. DPP alipinga ombi hilo kwa maslahi ya nchi.
Wakili Rweyongeza alidai kuwa katika hati ya kuzuia dhamana, DPP ametumia Sheria ya Mwenendo wa Mkakosa ya Jinai (CPA) badala ya Uhujumu Uchumi, ambayo ndiyo wanashitakiwa nayo washitakiwa hao pia alipaswa kuliwasilisha baada ya upelelezi kukamilika.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali Faraja Nchimbi anayemuwakilisha DPP, alidai Sheria zote zinaweza kutumika na DPP anaruhusiwa kuwasilisha hati hiyo wakati wowote.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili wakati wa usikilizwaji waombi la dhamana hiyo, Jaji Rose Teemba alisema atatoa uamuzi keshokutwa.
Washitakiwa katika kesi hiyo ni Huang Gin (50), Xu Fujie (22) na Chen Jinzhan (31), kwa mara ya kwanza walipandishwa kizimbani Novemba 9 mwaka huu.
Wakati hayo yakiendelea katika Mahakama Kuu, jana kesi hiyo ilitajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kuahirishwa hadi Desemba 30 mwaka huu itakapotajwa tena.
Washitakiwa wanadaiwa Novemba 2 mwaka huu katika eneo la Mikocheni B, walikamatwa na nyara za Serikali ambazo ni vipande 706 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 1,889 vyote vikiwa na thamani ya Sh bilioni 5.4 mali ya Serikali bila kuwa na kibali.