WANAMGAMBO WA KIISLAMU WAUAWA HUKO NIGERIA

Msemaji wa jeshi la Nigeria amesema kuwa wanamgambo hamsini wa Kiislamu waliuawa siku ya Jumatatu, wakati walipokuwa wakijaribu, kuvuka mpaka na kuingia taifa jirani la Cameroon.

Tukio hilo lilitokea baada ya wapiganaji wa Boko Haram, kushambulia kituo kimoja cha kijeshi Kaskazini Mashariki mwa mji wa Bama siku ya Ijumaa.

Waasi hao wenye msimamo mkali, walitoroka mji huo huku wakiwa wamewateka nyara wanawake na watoto.

Wanajeshi kumi na watano wa serikali na raia watano pia waliuawa.

Jeshi la Nigeria limekuwa likifanya operesheni ya kuwasaka wapiganaji hao wa Kiislamu, Kaskazini Mashariki na nchi hiyo tangu mwezi Mei mwaka huu, wakati serikali ilipotangaza hali ya hatari katika eneo hilo.

Kwa wakati huo, wapiganaji wa Boko Haram, walikuwa wametimuliwa kutoka miji mikuu, lakini mashambulio yaliendelea zaidi katika maeneo ya vijijini.