MANGARIBA 38 WAKAMATWA

Afisaa mmoja wa serikali kaskazini mwa Tanzania ameambia BBC kuwa kikundi kikubwa cha watu waliokamatwa kwa kuhusika na ukeketaji wa wasichana mjini Moshi watafikishwa mahakamani Jumatano.

Kamishna wa wilaya katika eneo la Kilimanjaro (Herman Kapufi,) amesema kuwa watu 38 waliokamatwa Jumatatu miongoni mwao ni wazazi wa wasichana waliokuwa wanakeketwa.

Alisema kuwa wasichana waliokeketwa wanapokea matibabu.

Maafisa wakuu mjini Moshi Tanzania, waliwakamata wanawake 38 mnamo siku ya Jumatatu waliopatikana wakiwakeketa wasichana katika eneo hilo.

Haijulikani idadi ya wasichana walioathirika. Lakini ripoti zinasemakuwa walikuwa kati ya umri wa miaka 3 na 16.

Ingawa ukeketaji ambao umeharamishwa huendelezwa katika sehemu nyingi za Mara na Dodoma nchini Tanzania , hilo sio jambo la kawaida kutokea mjini Moshi.

Inaarifiwa wanawake hao walikamatwa walipokuwa wanacheza dansi ya kitamaduni wakiwazingira wasichana ambao ndio walikuwa wamekeketwa tu.Baadhi ya wasichana inaarifiwa badowalikuwa wanavuja damu na wengine wakiwa wanauguza majeraha.

Ukeketaji umeharamishwa nchini Tanzania tangu mwaka 1998 ingawa bado unaendelezwa katika baadhi ya sehemu za nchi hiyo.

Inakisiwa asilimia 15 ya wasichana pamoja na wanawake wamekeketwanchini humo.