WAASI 19 WA LRA WAKAMATWA

Jeshi la Uganda linadai kuwa limewakamata waasi 19 na kumuua kamanda mmoja kwa jina Kanali Samuel Kangul.

Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi, msemaji wa jeshi la Uganda Luteni Kanali Paddy Ankunda, amesema kuwa waasi hao kumi na tisa waliokuwa wanaongozwa na kamanda Obur Nyeko walijisalimisha pamoja na bunduki 9aina ya SMG.

Ankunda amesema kuwa wote waliojisalimisha ni raia wa Uganda wakiwemo watoto 6 waliokuwa wanatumika kama wapiganaji wa kundi la LRA.

Jeshi la Uganda likishirikiana na kikosi cha Muungano wa Afrika, wamekuwa wakiendesha harakati zakuwasaka waasi wa LRA baadhi yao wakiwa wanatakiwa na mahakama ya uhalifu wa kivita ya ICC kama kiongozi wao Joseph Kony.

Bwana Ankunda amenukuliwa akisema kuwa jeshi la Uganda litaendelea kuwapokea waasi wanaoasi vita.

''Tukiendelea kufanya kazi kuambatana na sheria za kimataifa tuko tayari kuwapokea waasi wote wanaorejea nyumbani,'' alisema Ankunda.