Amewasamehe kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, iliyotolewa jijini Dar es Salaam jana.
Alisema ni mategemeo ya Serikali, kwamba watakaoachiwa huru, watarejea katika jamii kushirikiana na wananchi wengine katika ujenzi wa Taifa na watajiepusha na makosa ili wasirejee tena gerezani.
Alisema katika msamaha huo, wafungwa wote wapunguziwe mojaya sita ya vifungo vyao zaidi ya punguzo la kawaida, lililotolewa chini ya Kifungu 49(1) cha Sheria yaMagereza Sura ya 58, isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika Ibara ya 3(1-xiii).
Aidha, alisema msamaha huo, unawahusu wafungwa wagonjwa wenye magonjwa ya kifua kikuu, kansa na Ukimwi ambao wako kwenye hatua za mwisho na wamethibitishwa na jopo la waganga, chini ya uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa au Mganga Mkuu wa Wilaya.
Wengine ni wafungwa wazee wenye umri wa miaka 70 au zaidi ; na umri huo umethibitishwa na jopo la waganga, chini ya Uenyekitiwa Mganga Mkuu wa Mkoa au Mganga Mkuu wa Wilaya.
Pia, msamaha huo unawahusu wafungwa wa kike, walioingia na mimba gerezani, pamoja na wale walioingia na watoto wanaonyonyesha na wasionyonyesha.
Wengine waliopata msamaha huo ni wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili ;na ulemavu huo uwe umethibitishwa na jopo la waganga, chini ya uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa au Mganga Mkuu wa Wilaya.
Dk Nchimbi alisema msamaha huowa Rais, hauwahusu wafungwa waliohukumiwa kunyongwa na wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kifo na adhabu hiyo kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha gerezani.
Pia, msamaha huo hauwahusu wafungwa wanaotumikia kifungo cha maisha, wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, ikiwemo cocaine, heroin na bangi.
Wengine ni wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kupokea au kutoa rushwa, wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya unyang'anyi na unyang'anyi wa kutumia silaha, wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kupatikana na risasiau silaha.
Msamaha huo pia hauwahusu wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kunajisi, kubaka na kulawiti, wanaotumikia kifungo kwa makosa ya wizi wa magari wa kutumia silaha na wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka yao.
Aidha hauwahusu wafungwa waliohukumiwa kifungo kwa kosa la kuwapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na shule za sekondari ;na ambao walitenda kosa hilo wakiwa na umri wa miaka18 na kuendelea.