Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu na kuchapishwa katika gazeti la Sudan Tribune, mwenyekiti huyo amesema ana wasiwasi hasa na hali ya usalama wa wananchi.
Mapigano yalizuka katika mji wa Juba, Jumapili jioni kati ya vikundi vyenye silaha katika kambi ya jeshi na mapigano hayo yaliripotiwa kuendelea Jumanne, huku milioni ya bunduki ikisikika katika maeneo yote ya mji wa Juba mbali na kuhakikishiwa na serikali ya Sudan Kusini kuwa imedhibiti hali hiyo.
Dlamini-Zuma ameitaka serikali ya Sudan Kusini na makundi mengine yanayohusika katika mapigano hayo kujizua na aina yoyote ya kuendelea kwa mgogoro huo.
Pia amezitaka pande zinazohusika na mgogoro huo kutafuta suluhisho la amani kutokana na tofauti zao, "kwa kuheshimu utawala wa sheria, haki za binadamu na uhalali wa kikatiba", akisema AU iko tayari kusaidia kutafuta suluhisho la hali ya sasa.
Wito wa AU umekuja wakati Marekani ikizitaka pande zinazohusika katika mgogoro wa Sudan Kusini kujizuia na ghasia nakutafuta suluhisho la amani.
Mjumbe maalum wa Marekani Donald Booth alitumia mawasiliano ya Twitter siku ya Jumatatu akitaka kuwepo kwa haliya utulivu, akisema migogoro ya kisiasa lazima imalizike kwa njia ya mazungumzo na sio vurugu.
Rais Salva Kiir amemshutumu naibu wake wa zamani, Riek Machar, kwa kuchochea jaribio la kutaka kuiangusha serikali yake.
Mawaziri kadha wa zamani wamekamatwa, wakihusishwa na jaribio hilo, ambapo mawaziri wengine hawajulikani walipo.
Bwana Kiir ametangaza amri ya kutotembea ovyo usiku katika mji wa Juba, ambapo maeneo mengi yenye pilikapilika za kibiashara, yamekimbiwa kwa kiasi kikubwa.
Hata hivyo, mazingira ya jaribio hilo hayako bayana, huku kukiwa na taarifa zinazokinzana na kauli rasmi ya serikali kuhusu tukio hilo, zikidai kuwa msuguano wa uongozi katika chama tawala, SPLM katika wiki za karibuni ulisambaa hadi katika jeshi, SPLA, na kuchochea mapigano kati ya wafuasi wa Bwana Kiir na Machar.
Jumatatu, walinzi wa rais waliizingira nyumba ya Bwana Machar katika eneo la Amarat, nakuharibu sehemu kubwa ya nyumba hiyo. Hakuwa nyumbani wakati huo na mpaka sasa hajulikani alipo.
Maafisa wa afya wanasema watu wapatao 26 wamethibitika kufariki dunia katika hospitali ya Juba, wakati zaidi ya watu 113 wametibiwa kutokana na majeraha ya risasi.