CHEKA ACHEZEA KICHAPO KWA KO

BONDIA Francis Cheka juzi alichezea kichapo cha KO kutoka kwa Fedor Chudinov wa Urusi na kuvuliwa rasmi mkanda wa WBF alioupata baada ya kumpiga bondia Phil Williams wa Marekani kwenye pambano la lisilokuwa na ubingwa la raundi 8.

Mpambano huo ulifanyika Urusi katika Ukumbi wa Dynamo Palace, Krylatskoye ni wa kwanza kuchapwa baada ya kutawazwa kuwa bingwa wa WBF, mkanda ambao anaushikilia lakini kutokanana sheria za WBF ukipigwa kwa KO kwenye mpambano wa kirafiki unapoteza mkanda huo.

Kwa kipigo hicho Cheka ameporomoka kwenye viwango vya ubora vya WBF toka nafasi ya 20 hadi 48 na inamlazimu kufanya kazi ya ziada kuhakikisha kuwa anaomba kugombea mkanda wa WBF kabla ya Januari mwakani.Akizungumza kwa masikitiko promota J. Msangi alisema kuwa Cheka hakupaswa kupigana pambano kama hilo kwani alikuwa hajajiandaa vya kutosha na bado yeye alikuwa anamwandalia pambano ambalo angepigana Februari, mwakani.

"Cheka alipokuwa amefikia hakupaswa kupigana mapambano ya kulipwa dola 10,000, kwa sasa yeye anatakiwa kupigana pambano ambalo anatakiwa kulipwa kuanzia dola 30,000 hadi 60,000 lakini nimesikitika zaidi baada ya kusikia kapigwa kwa KO raundi ya tatu na kupoteza mkanda wake," alisema Msangi.

Pia Msangi alisema kuwa watawasiliana na WBF kuomba Cheka agombanie huo mkanda hapa nchini mapema Januari 24, mwakani ili iwe rahisi kwake kushinda.

Katika pambano hilo bondia mwingine wa Tanzania Allan Kamote naye alipigwa kwa KO raundi ya saba kwenye pambano ambalo lilikuwa la raundi tisa.

Taarifa zilizopo kwa mwaka huu mabondia 16 waliokwenda kucheza nje ya nchi hakuna hata mmoja aliyeshinda jambo ambalo linaacha maswali mengi kwa wadau wa ngumi.