Kwa mujibu wa taarifa, mke wa Thamsanga Jantjie, Siziwe, alimpeleka mumewe katika Hospitali ya Krugersdorp Jumanne,kufanyiwa vipimo, lakini ikapendekezwa alazwe mara moja.
Mkalimani huyo wa lugha ya alamakatika kumbukumbu hiyo, amelazwa katika Hospitali ya wagonjwa wa akili ya Sterkfontein, gazeti la The Star la Afrika Kusini liliripoti jana.
"Siku chache zilizopita, zilikuwa ngumu. Tumekuwa tukiishi kwa hadhari kubwa kwa sababu wakati wowote angeweza kuharibikiwa," aliongeza Siziwe. Jantjie alipaswa Desemba 10 awe amepelekwa Sterkfontein kwa ajili ya uchunguzi wa afya.
Hata hivyo, baada ya kupata 'dili' yakufanya ukalimani katika ibada ya kumbukumbu ya Mandela kwenye uwanja wa FNB siku hiyo, Jantjie aliwasiliana na hospitali ili kubadilisha miadi yake.
Juzi, Waziri wa Ofisi ya Rais, Collins Chabane alisema Serikali itachunguza madai kuwa Jantjie hakutumia ukalimani mwafaka siku hiyo.
Baada ya shughuli hiyo, Jantjie aliviambia vyombo vya habari kuwa ana matatizo ya uchizi na sikuhiyo alijikuta akiona maluweluwe wakiwamo malaika wakishuka, na kwamba alipatwa kiwewe alipogundua kuwa alikuwa amezungukwa na polisi wenye silaha.
Familia ya Mandela Wakati huo huo, mjane wa Mandela, Winnie amekanusha kuwapo kwa mzozo ndani ya familia ya kiongozi huyo wa zamani.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo mbalimbali, inadaiwa kwamba mjukuu mkubwa wa Mandela, Mandla ambaye ni mrithi wa uchifu wa ukoo wa Madiba ametengwa na familia hiyo.
Lakini Winnie alikanusha uvumi huo potofu aliouita ni "staili ya ubaguzi wa rangi." "Habari, taarifa na tahariri za vyombo vya habari…zinasema familia ya Mandela iko vitani tangu habari za kwanza kwamba Madiba hayuko nasi tena," alisema msemaji wake, Thato Mmereki katika taarifa yake.
"Taarifa hizi hazijafanya lolote zaidiya kuja na ukweli nusu nusu kwa lengo la kuichafua familia ya Mandela katika kipindi hiki kigumucha maombolezo."
Kwa mujibu wa vyombo vya habari ndani ya Afrika Kusini, vitasa vya nyumba ya Mandela iliyoko Estern Cape vilibadilishwa baada ya bintiye mkubwa, Makaziwe, kuwasili hapo Alhamisi – wiki moja baada ya kifo cha baba yake na sikutatu kabla ya maziko.
Maji na umeme vilikatwa siku ya mkesha wa maziko ya Mandela kijijini Qunu Jumapili ukiwa ndio mwisho wa siku 10 za maombolezo ambayo yalifuatiliwa na mamilioni ya watu duniani.
Makaziwe inasemekana alisimamia maandalizi ya mazishi, huku Mandla akionekana kiongozi wa familia-akisimamia jeneza lenye mwili wa babu yake katika siku zote tatu za kuagwa katika majengo ya Serikali ya Union jijini Pretoria, wiki jana.
Mandla, akishutumu baadhi ya shangazi zake kwa kujaribu kudhibiti fedha za Mandela, alipata kuhamisha mabaki ya marehemu baba yake, Makgatho, ambaye alifariki dunia kwa Ukimwi mwaka 2005 na watoto wengine wawili wa Mandela kutoka Qunu kuyapeleka Mvezo ambako Mandela alizaliwa.
Familia yake ilidai, kwamba huo ulikuwa mpango wa kulazimisha maziko ya Mandela yafanyikie Mvezo – kwa kuwa Mandela katika wosia wake alitaka azikwe karibu na makaburi ya wanawe hao-kwa lengo la kuvutia utalii.
Mandla hatimaye alilazimishwa na Mahakama kurudisha mabaki hayo Qunu. Winnie alisema juzi, kwamba, "hakuna mgogoro wala majadiliano ya urithi ndani ya familia ya Mandela. Na kwa mujibuwa sheria za kimila na utamaduni binti mkubwa, ambaye ni Makaziwe, ataongoza familia na kuchukua uamuzi akishirikiana na wadogo zake wa kike.
"Mandla anaheshimiwa kama mmoja wa wajukuu wa Mandela, kizazi kijachocha familia ya Mandela."