SNOWDEN ASEMA LENGO LAKE LIMEKAMILIKA

Mfanyakazi wa zamani wa muda katika Shirika la Usalama la Marekani, NSA, Edward Snowden, ambaye alifichua kuwepo kwa mipango ya Marekani kufuatilia taarifa za mawasiliano ya watu, amesema amefaniskisha lengo lake.

"Kwa kuridhika binafsi, mpango wangu tayari umefanikiwa," ameliambia gazeti la Washington Post.

"Tayari nimeshinda," amesema Bwana Snowden, ambaye ufichuaji wake mkubwa umesababisha Marekani kuangalia upya sera yake ya ufuatiliaji wa taarifa za siri za watu na mashirika.

Snowden mwenye umri wa miaka30, alifanya mahojiano na gazeti hilo nchini Urusi, ambako alipewa hifadhi ya ukimbizi wa muda tarehe Mosi Agosti.

Bwana Snowden aliondoka Marekani mwishoni mwa mwezi Mei, akichukua kiasi kikubwa cha nyaraka za siri kuhusu mpango wa udukuzi wa Marekani.

Anakabiliwa na mashitaka ya ujasusi nchini Marekani.

NSA iligundulika kuhusika katika udukuzi wa data za simu. Taarifa za kina za watu na taasisi zilizolengwa na udukuzi wa mashirika ya ujasusi ya Uingereza na Marekani zilichapishwa wiki iliyopita na magazeti ya The Guardian, The New York Times na Der Spiegel.

Magazeti hayo yamesema orodhaya watu na taasisi zipatazo 1,000 zilizolengwa ni pamoja na Kamishna wa Umoja wa Ulaya, mashirika ya kibinadamu na maafisa wa Israel akiwemo waziri mkuu.

Makampuni makubwa ya teknolojia ya mawasiliano nchini Marekani ya Google, Microsoft na Yahoo yanachukua hatua ya kuzuia ukusanyaji wa data unaofanywa na serikali yao.

Mwezi Oktoba, habari ziliposambaa kuwa NSA lilikuwa limedukua mazungumzo ya simu ya kiongozi wa Ujerumani Chansela Angela Merkel, kulisababisha mvutano wa kidiplomasia kati ya Ujerumani na Marekani.

Rais wa Brazil Dilma Rousseff naye pia alikasirishwa na taarifa kwamba shirika la ujasusi la Marekani, NSA, liliingilia mtandao wa kompyuta wa kampuni ya mafuta ya serikali ya Brazil, Petrobras ili kukusanya taarifa na mawasiliano ya barua pepe na simu.