TANESCO KUPANDISHA BEI YA UMEME 2014

Watanzania wanataraji kuuanza mwaka 2014 kwa machungu ya kupanda kwa bei ya umeme, ambapo (leo) mamlaka ya udhibitiwa nishati na maji, EWURA imetangaza rasmi ongezeko la gharama za nishati hiyo kwa asilimia 39.19, kuanzia January mosi, mwakani.

Bei za umeme zinazotumika hivi sasa ziliidhinishwa January mwaka2012, ambapo zilipanda kwa asilimia 40.29, ikilinganishwa na maombi ya shirika la umeme, TANESCO lililopendekeza kupanda kwa bei kwa asilimia 155.

Watumiaji wakubwa wa umeme wa majumbani, biashara na viwanda vidogo vidogo, ambao wako kwenye kundi la wateja la T1, wanatarajia kuathirika zaidi ambapo ongezeko kwenye kundi hilo ni shilingi 85 kwa kila unit.

Kundi la T3-MV lenye wateja wakubwa waliounganishwa katika msongo wa kati, bei ya nishati imeongezeka kwa shilingi 45 na kundi T3-HV la wateja waliounganishwa kwenye msongo wa juu wakiongezewa kwa shilingi 53 kwa unit.

Kwa mujibu wa TANESCO, maombi haya yanalenga kuliwezesha shirika kupata fedha za uendeshaji na uwekezaji wa miundombinu, kujiwezesha kukopesheka kwa masharti nafuu,kuweza kukabili ongezeko la mahitaji ya umeme kwenye gridi ya taifa na uwezo wa kufanya marekebosho ya miundombinu yamara kwa mara.

Hasara kwenye shirika hilo la TANESCO linalojiendesha kwa hasara hivi sasa imefikia shilingi Bilioni 223.4, toka Bilioni 47.3 la mwaka 2010, na deni la zaidi ya shilingi Bilioni 400, huku pia shirika likigubikwa na kashfa ya ubadhirifu wa fedha.

Agizo hili la kupanda kwa bei za umeme, linafuta agizo la January 24, 2013 la TANESCO linalohusu marekeboshi ya bei za umeme.