PINDA: TANZANIA ISITEGEMEE WAFADHILI

Suala la baadhi ya wafadhili wa Tanzania kubana au kuchelewesha fedha walizoahidi kusaidia bajeti ya nchi hiyo kumeendelea kuiumiza serikali.

Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda, amesema umefika wakati sasa kwa Tanzania kujitegemea kwa mapato ya ndani kwa asilimia 100 badala ya kutegemea wahisani ambao amedai wanakuwa na maslahi yaokatika kusaidia.

Hivi karibuni wahisani wamesitisha kutoa fedha hizo kuishinikiza Tanzania kuchukua hatua dhidi ya upotevu wa mabilioni ya fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania katika mazingira yanayodaiwa kuwa ya rushwa.

Kiongozi huyo mwandamizi wa serikali ya Tanzania ametoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kurejea kutoka ziara ya ughaibuni ambako alihudhuria mikutano katika nchi mbali mbali akishughulikia masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na uwekezaji.

Japo kuwa Waziri Mkuu Pinda hafafanui kwa nini serikali haichukui hatua za haraka kukamilisha uchunguzi wa upotevu wa takriban dola milioni 120 kutoka Benki Kuu ya Tanzania katika mazingira yanayodaiwa kugubikwa na rushwa kubwa, amesema wahisani hao wasingeisumbua Tanzania kama ingekuwa inajitegemea asilimia 100 kutokana na mapato ya ndani ya nchi.

"Ukishakuwa tu ni mtu ambaye unaonekana wewe bila wao taabu, ndiyo shida inaanzia hapo.
Ndiyo maana wakati mwingine inabidi kusema bwana sisi tujitahidi, TRA huyu huyu twende naye akiweza kuongeza zaidi kidogo basi tutamshukuru sana.
First and foremost tumtumie yeye na tuone hiki kidogo tunachokipata kutoka TRA tunavyoweza kukitumia vizuri zaidi kutupunguzia matatizo yetu.
Kama zikija hizo nyingine well and good lakini si option ambayo unasema inakupa faraja kubwa sana. kwa sababu anything jambololote likitokea wanabana tu, halafu matokeo yake inakuwa ovyo sana katika shughuli zenu zamaendeleo," alieleza Bw Pinda.

Ingawa kauli yake haitapunguza maumivu ya wananchi wanaosubiri huduma na utekelezaji wa miradi ambayo ilishapangwa, pia ni vigumu kufanikisha jambo analolisema kwa muda mfupi.

Waziri Mkuu Pinda alipoongea na BBC hivi karibuni alikiri kwamba madai hayo ya utoroshaji wa fedha ni jambo linaloitia doa serikali ya Tanzania.

Swala hilo linaonyesha kuiumiza kichwa serikali wakati hasa kutokana na shughuli nyingi za maendeleo kuchelewa au kukwama, huku ikijikuta ikiwa haina njia nyingine ya haraka kurekebisha hali ya mambo.

Hata hivyo Waziri wa Fedha na Uchumi, Saada Mkuya Salum, akizungumza mjini Dar es Salaamamesema baadhi ya wahisani wamekwishatoa fedha na mazungumzo yanaendelea na waliobaki.

Ripoti ya uchunguzi unaofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambayo imekuwa ikifanya kazi hiyo kwa miezi kadhaa inasubiriwa kwa hamu ili ibainike endapo kulikuwa na hila katika kuchomolewa fedha zilizokuwa zimewekwa kwenye akaunti maalum katika Benki Kuu ya Tanzania kusubiri usuluhishi wa suala la kibiashara umalizike.